November 04, 2023

HAKUNA MWANACHI KUTOZWA FEDHA ZA HUDUMA - RC SENYAMULE






Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amekemea tabia ya baadhi ya Viongozi wa Kata na vijiji wanaowatoza wananchi fedha kwa ajili ya kuwapatia huduma. Hayo yamesemwa wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Kijiji cha Kinusi kilichopo kwenye Kata ya Ipera, tarafa ya Rudi, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Novemba Pili, 2023.

Ziara hiyo yenye lengo la kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ambapo ni muendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa kutembelea miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Akijibu kero mbalimbali zilizowasilishwa mbele yake, Mhe. Senyamule amekemea rushwa kwa viongozi wa Kata na Vijiji kwani huduma bure ni haki ya mwananchi.

"Hakuna mwananchi kuombwa fedha kwa ajili ya kupatiwa huduma kwa mtendaji wa Kijiji kwani huko ni kuichafua Serikali. Viongozi munapata mishahara na posho kwa ajili ya matumizi yenu ya ziada kila mwezi na haya yote yamefanywa na Serikali ili wananchi wapate huduma bure Mana ndio tamaa ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ladha ya Mhe. Rais ni kugusa maisha ya wananchi wa chini kutokana na shida zao hivyo hatutasita kuwachukulia hatua viongozi watakaobainika kufanya hivyo" Amesema Mhe. Senyamule

Mbali na kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Mhe. Senyamule amesisitiza mambo kadhaa kwa watendaji wa Halmashauri ya Mpwapwa ikiwa ni pamoja na viongozi wa vijiji kufanya vikao vya kuwasilisha kwa wananchi, wazazi na walezi kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kuanza shule wanapelekwa shule kwani Serikali imejenga madarasa ya kutosha na mwisho amesisitiza utunzaji wa mazingira kwa wakazi wa Kata ya Ipera kwa viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia kampeni ya kupanda miti mitano kwenye kila kaya ili kuzuia athari za mmomonyoko wa udongo pamoja kuikijanisha Dodoma.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo, amewataka wananchi kusimamia na kuilinda miradi inayoanzishwa kwenye maeneo yao kwa kuwa Ina manufaa kwao pindi itakapokamilika.

"Tusimamie miradi inayoanzishwa kwenye maeneo yetu ikiwemo ujenzi wa kituo hiki cha afya cha Ipera Mana ni cha wananchi, tukisimamie ili kijengwe kwa ubora kwa kuhakikisha tunalinda vifaa vya ujenzi visiibiwe. Pia nitashughulikia wale wote watakaobainika kufanya wizi kwenye miradi hii ya Serikali kwa kuwachukulia hatua" Amesisitiza Mhe. Kizigo

Aidha, Diwani wa Kata hiyo Bw. Festo Sugala Myuguye, amebainisha miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Kata yake ambayo inagharimu kiasi cha fedha shilingi Bilioni 3.2 ambayo ni ujenzi wa madarasa 6 ya UVIKO na Ofisi, matundu 13 ya vyoo, madarasa yaliyogharimu shilingi Milioni 600, matundu 8 ya vyoo kwa kiasi cha Shilingi Milioni 8, Madawati shilingi Milioni 2.4, pia fedha zinaletwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama, mradi wa skimu ya umwagiliaji shilingi Milioni 135, kituo cha afya shilingi Milioni 500 na Barabara ya zege umbali wa Km 1 unaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1 na Milioni 385.

No comments:

Post a Comment