Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Marekani ukiongozwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle kuhusu mikakati mbalimbali ya kukuza Sekta ya Utalii, pamoja na uhifadhi wa wanyamapori .
Kikao hicho kimefanyika leo Oktoba 24,2023 katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Jengo la Mpingo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Kairuki amemuomba Balozi Battle kuhamasisha wawekezaji wakubwa kutoka nchini Marekani kuwekeza nchini Tanzania .
“Ninaomba uhamasishe wawekezaji wakubwa nchini Marekani kuja Tanzania kuwekeza katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya utalii hasa katika huduma ya malazi kwa kujenga hoteli, kambi za watalii, huduma za usafiri na nyinginezo.
Amefafanua kuwa kutokana na idadi ya watalii kuendelea kuongezeka Tanzania imekuwa na upungufu wa vyumba vya kulala wageni.
Aidha, amemuomba Balozi huyo kuendelea kufadhili miradi ya kupambana na ujangili, na uwekezaji katika uchumi wa kijani “Green Investment”unaohusisha biashara ya hewa ukaa, upandaji miti, misitu, mimea vamizi kama mikoko ili kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mhe. Michael Battle amesema Marekani imekuwa ikiwezesha miradi mbalimbali ya Maliasili na Utalii akitolea mfano Mradi wa Kukabiliana na Ujangili ambapo ilikabidhi vitendea kazi , vifaa, mafunzo ya kujengea uwezo na ufadhili kwa Kikosi kazi cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ujangili.
Ameongeza kuwa nchi yake imekuwa ikifadhili programu mbalimbali nchini kwa kufanya kazi na hifadhi za Serengeti, Ngorongoro, Mkomazi na Ruaha.
Ushirikiano wa Tanzania na Marekani umezidi kuimarika na hivyo kusaidia kukuza sekta ya utalii nchini.
No comments:
Post a Comment