October 31, 2023

RAIS WA IPU AWAOMBA WATANZANIA USHRIKIANO ILI KUONESHA UTOFAUTI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Rais wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Katikati ni Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko. 
*****************
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ameomba ushirikiano kutoka kwa Watanzania wote ili kuionyesha Dunia utofauti wa Tanzania kuishika nafasi hiyo.

 
Dkt. Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania ametoa kauli hiyo leo Bungeni Dodoma katika halfa ya kumpokea akitokea Nchini Angola ambako alishinda nafasi ya Rais wa IPU katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 2023.
 
Amesema Tanzania inayo nafasi ya kufanya vizuri katika nafasi hiyo iwapo kutakuwepo ushirikiano kutoka kwa watu wote.
 
“Nafasi hii ni yetu wote, ukiwa na ushauri wa namna ya kuupeleka umoja huu mbele tuletee ili tufanye vizuri, usisuburi tushindwe.
 
“Ifike mahali tukitaka nafasi nyingine kimataifa tupate kwa kuwa tulifanya vizuri kwenye hii, tutasikiliza ushauri wenu, ninaamini tutafanya vizuri na Dunia itajua kwamba tulishawahi kushika hii nafasi, viongozi wa dini muendelee kutuombea,” alisema.
 
Alitoa wito kwa Watanzania kuondoa tofauti zao kwenye masuala ya uwakilishi wa Tanzania Kimataifa kwa kuacha kuidharau nchi mbele ya nchi nyingine.
 
“Nafasi kama hizi siyo za kuzipiga teke, tujitahidi kujizuia hasa katika mambo ya kimataifa, tusifike mahali ya kuiuza au kuidharau nchi yetu kwa wengine, usiungane na adui kwa ajili ya kulipiga Taifa lako,” alisema.
 
Mheshimiwa Dkt. Tulia alitoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuwesha kupita katika mchakato wa uchaguzi uliodumu kwa miezi mingi na kwamba isingiwezekana bila yeye kutoa kibali.
 
“Vilevile namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Hasan Suluhu kwa kuridhia nigombee nafasi hii, nafasi kama hii huwezi kugombea bila nchi yako kuruhusu na anayeruhusu ni Mheshimiwa Rais.
 
“Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuridhia Bunge la Tanzania kuchukua nafasi hii, pia niwashukuru wote walioshiriki kwa nafasi yao, kwa maombi, maoni, kututia moyo na michango ya kifedha pamoja na waliotukatisha tamaa kwa kuwa ilitufanya tupige hatua kwa haraka zaidi” alisema.
 
Alisema Mheshimiwa Rais pamoja na kutoa usafiri wa ndege kumrudisha Tanzania, lakini pia ametoa ushirikiano mkubwa ambao ndiyo umemfikisha hapo toka mchakato wa uchaguzi  ulipoanza.
 
“Hatukuwa peke yetu, wapo marafiki wengine walikuja kutusaidia ili tushinde nafasi hii, tumeungwa mkono na mataifa mengi kwa kuwa wanaamini sera za nchi yetu ambazo zinaendana na misingi ambayo IPU inaisimamia,” alisema
 
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Tulia alieleza historia yake kwa ufupi akitambua mchango wa Mheshimiwa Balozi Dkt. Asha Rose Migiro katika mafanikio yake huku akiahidi kuandika kitabu.
 
Waziri Mkuu
Awali Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa  akitoa salamu za Serikali alisema
Mheshimiwa Rais Samia Hasan Suluhu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango wanampongeza kwa ushindi mnono wa nafasi hiyo nyeti.
 
“Sisi tumefarijika kama Serikali kwa sababu moja kati ya majukumu yako utakuwa unashiriki vikao vyote vya Umoja wa Mataifa, tunayo mikataba mingi katika nyanja za kimataifa, tutakutumia wewe kuingiza ajenda za nchi.
 
“Tuna uhakika utatupigania, tulikuwa tunakufuatilia katika mchakato wa kuomba kura, kazi kubwa mmeifanya leo tunifurahia kazi hii.
 
“Mheshimiwa Rais amefurahishwa na akaamua kukuletea ndege kubwa kwa ajili yako na kwa ajili ya ya heshima uliyoileta nchini. Naahidi Serikali itashirikiana na wewe kila hatua, na maeneo ambayo utahitaji Serikali ikupe taarifa kwa ajili ya kwenda kufanyia kazi huko katika majukumu yako tutakupatia,” alisema.
 
 
Naibu Spika
Mheshimiwa Naibu Spika, Mussa Azan Zungu alisema mambo matatu ndiyo yalimfanya Mheshimiwa Dkt. Tulia kushinda nafasi hiyo ambayo ni kujiamini, heshima na ukweli huku akisema jambo kubwa zaidi ni kumuamini Mwenyezi Mungu na msaada kutoka kwa Mheshimiwa Rais.
 
“Sisi tuliogopa uchaguzi lakini Mungu alishasema tunashinda, you deserved it (ulistahili) na umefanya kazi kubwa sana,” alisema.
 
Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu CCM, Zanzibar, Dkt. Mohammed Said Mohammed aliungana na wengine wote kumpongeza Dkt. Tulia kwa kuwa Rais IPU wa kwanza mwanamke kutoka Afrika.
 
CCM imefarijika sana kupata kiongozi katika nafasi hiyo, nifahari kubwa kwa wanawake wote Barani Afrika hususan wanawake wa Chama Cha Mapinduzi, kuchaguliwa kwa Dkt. Tulia kunaiweka Tanzania kileleni katika ramani ya Dunia kwenye masuala ya demokrasia na usawa wa binadamu kwa kuwa mwanamke kashika nafasi hiyo,” alisema.
Katibu wa Bunge.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimpongeza, Rais wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa kuteuliwa kua Rais wa Mabunge Duniani (IPU), katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko, akimpongeza, Rais wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa kuteuliwa kua Rais wa Mabunge Duniani (IPU), katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.




No comments:

Post a Comment