Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa
kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika shule za msingi mkoani Singida
uliofanyika Oktoba 24, 2023 mkoani Singida.
Wengine
kutoka kushoto ni Meneja MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, Mkuu wa Wilaya
ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Lodovick
na Mwakilishi wa Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya
Afya , Theresia Shirima. Vyandarua hivyo vitasambazwa na MSD katika shule hizo.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya
viongozi walioshiriki uzinduzi huo.
Na
Dotto Mwaibale, Singida
BOHARI
ya Dawa (MSD) imeanza kusambaza vyandarua zaidi ya 341,000 vyenye dawa katika
shule za msingi mkoani Singida kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo
2030.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika shule za msingi
mkoani Singida, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi
hiyo ya usambaji wa vyandarua hivyo itafanyika kwa wiki tatu.
Alisema
MSD ndio yenye mamlaka ya kisheria ya
Kununua, Kuzalisha, Kuhifadhi na Kusambaza bidhaa za Afya hapa nchini ndio
maana wanafanya kazi hiyo.
Alisema
MSD wanasambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara na kuwa vyandarua
vinaingia kama vifaa tiba ambavyo vinatumika kumkingia mwananchi asishambuliwe
na malaria.
“MSD
leo tupo mkoani Singida kushuhudia uzinduzi wa usamabazi wa vyandarua zaidi ya
341,000 kwenye shule za msingi katika halmashauri za wilaya sita isipokuwa moja
ya Singida Manispaa na hilo ndilo jukumu tulilopewa na zoezi hili la ugawaji wa
vyandarua hivi tunatarajia kulifanya kwa kipindi cha wiki tatu,” alisema Jumaa.
Alisema
ili zoezi hilo liweze kukamilika wanahitaji kupata ushirikiano kwa wadau wote
ambao ni sehemu ya usambazi huo ambao ni wakuu wa wilaya, wakurugenzi, maafisa
elimu kuanzia mkoani hadi kwenye kata na wakuu wa shule na kwa ushirikiano huo
unaweza kuwafikisha kwenye lengo walilojiwekea.
Alisema
MSD imepewa jukumu hilo kutokana na uzoefu mkubwa walionao na kuwa na
miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ya kielektroniki kuanzia kuhifadhi hadi
usambazaji.
Mkuu
wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi akizindua kampeni
hiyo alisema ugonjwa wa malaria bado ni tatizo mkoani hapa kutokana na utafiti
uliofanyika mwaka 2022 ulioonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria
kipo wastani wa asilimia 1.5 ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni
asilimia 8.4 (TMIS 2022)
Alisema
Halmashauri ya Itigi inakiwango kikubwa zaidi ya maambukizi ya asilimia 9.8
ukilinganisha na Halmashauri ya Singida ambayo ina kiwango cha chini zaidi ya
asilimia 0.0 na kueleza kuwa Serikali bado inaendelea na juhudi za kuhakikisha
inatokomeza kabisa ugonjwa hatarai wa malaria kufikia 2030.
Mwakilishi
wa Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kutoka Wizara ya Afya , Theresia
Shirima alisema adhima ya Serikali ni kuhakikisha hadi ifikapo 2030 ugonjwa wa
malaria unatokomezwa kabisa kwa kufanya usafi, kuharibu mazalia ya mbu na njia
nyingine ikiwamo ya ugawaji wa vyandarua mashuleni ambapo wanafunzi watasaidia
kuvifikisha kwenye kaya wanazotoka.
Alisema
walengwa zaidi katika hizo kaya ni yale makundi ambayo yanakuwa kwenye hatari
ya kupata maambukizi ya ugonjwa huo ambao ni wajawazito na watoto walio chini
ya miaka mitano.
Afisa
Elimu Mkoa wa Singida, Dkt. Elpidius Baganda alisema vyandarua hivyo vinakwenda
kugaiwa katika shule 670 na alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali chini ya
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo ni muhimu kwa taifa.
No comments:
Post a Comment