SERIKALI YAWASHUKURU WABIA WA MAENDELEO KUSAIDIA USAMBAZAJI UMEME VIJIJINI
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga (kushoto),
akizungumza na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ilambabusungu, Kijiji cha Bubiki,
Wilaya ya Kishapu, Mkoani Shinyanga, Mwandu Fimbo (kulia) wakati wa ziara ya
Bodi ya Nishati Vijijini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme,
Septemba 7 mwaka huu. Wa pili – kulia ni Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa. ***************
Veronica Simba – Shinyanga
Serikali imewashukuru Wabia
mbalimbali wa Maendeleo kutokana na mchango wanaoendelea kutoa katika kuwezesha
utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga alitoa shukrani hizo Septemba 7
mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga.
Akishiriki katika ziara ya
Bodi ya Nishati Vijijini (REB) kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya
umeme vijijini, hususan mradi wa ujazilizi mkoani humo, Mhandisi Maganga
alibainisha kuwa Wabia hao wa Maendeleo wana mchango mkubwa katika kufanikisha
mradi husika.
Aliwataja Wabia hao kuwa ni
Serikali za Norway, Sweden pamoja na Umoja wa Ulaya ambao kwa umoja wao
wamefadhili shilingi bilioni 147 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi
Fungu la Pili A katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma,
Kilimanjaro na Tanga.
“Wamekuwa nasi bega kwa bega
kuhakikisha kwamba azma ya Serikali kuwapatia wananchi huduma mbalimbali
ikiwemo nishati ya umeme inafikiwa hivyo kupunguza hali ya umaskini katika
maeneo husika,” alisema.
Mhandisi Maganga aliongeza
kuwa, wajibu wa REA ni kuhakikisha msaada uliotolewa unatumika kama
ilivyokusudiwa na Wabia hao wa Maendeleo ili malengo yaliyodhamiriwa yaweze
kufikiwa.
Aidha, alitumia jukwaa hilo
kuwakaribisha kutembelea miradi waliyoifadhili katika maeneo mbalimbali nchini
ili wajionee maendeleo ya utekelezaji wake.
Bodi inaendelea na ziara
katika Mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi
inayotekelezwa kupitia REA.
No comments:
Post a Comment