Msajili wa Bodi ya Usajili wa
Wahandisi (ERB), Mha. Patrick Barozi, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari
(hawapo pichani), kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania kwa mwaka
2021 yatakayofanyika siku mbili kuanzia tarehe 02 hadi 03 Septemba 2021 katika
Ukumbi wa Dkt. Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Maadhimisho Siku ya Wahandisi Tanzania kwa mwaka 2021, Prof. Bakari
Mwinyiwiwa, akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu
maadhimisho hayo yatakayoanza tarehe 02 hadi 03 Septemba 2021 katika Ukumbi wa
Dkt. Jakaya Kikwete, mkoani Dodoma.
BODI ya Usajili ya Wahandisi
(ERB), imewasimamisha wahandisi 17 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria
kwa kukiuka maadili na taratibu za taaluma yao kwa kipindi cha mwaka wa fedha
2020/2021.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma
na Msajili wa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi
Tanzania kwa mwaka 2021 yatakayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 02 hadi
03 Septemba, 2021 katika Ukumbi wa Dkt. Jakaya Kikwete, mkoani humo.
“Wahandisi hawa 17
wamewajibishwa kwa mujibu wa makosa na adhabu wanazostahili kupewa mfano ikiwemo
kujihushisha na masuala ya rushwa, upendeleo wa kazi, kushindwa kusimamia miradi
na kusimamia baadhi ya miradi chini ya viwango”, amefafanua Mhandisi Barozi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho hayo, Prof. Bakari Mwinyiwiwa, amesema kuwa
zaidi ya wahandisi 600 wanatarajiwa kula kiapo cha utii katika Maadhimisho ya
Siku ya Wahandisi kwa mwaka 2021 ili kuhakikisha wahandisi nchini wanawajibika
vyema kwenye taaluma zao na utendaji wao wa kila siku.
Prof. Mwinyiwiwa amesisitiza
kuwa kiapo kitatumika dhidi ya mhandisi atakapovunja miiko na maadili ya
taaluma katika utendaji wake wa kazi na hivyo vyombo mbalimbali vya kisheria
vitatumia kiapo hicho kumchukulia hatua za kisheria.
“Kiapo kinamkumbusha mhandisi
kuzingatia thamani ya fedha, usalama wa maisha ya binadamu na mazingira,
kutoruhusu masuala ya jinai, dini, jinsia, ukabila, rangi na masuala ya kisiasa
katika utekelezaji wa kazi zao za kiuhandisi”, amefafanua Prof. Mwinyiwiwa.
Mkutano huo utakaobeba kauli
mbiu ya “Athari za Mapinduzi ya Nne ya
Viwanda kwenye Miundombinu na Viwanda kwa Uendelevu wa Uchumi wa Kati”
utashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Uganda,
Misri na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao ikiwemo nchi ya Afrika Kusini,
Rwanda, Botswana, DRC na Kenya.
No comments:
Post a Comment