Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, akihutubia wanakijiji
wa kijiji cha Kidunda, Kata ya Mkulazi, Tarafa ya Ngerengere mkoani Morogoro
wakati wa ziara yake na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama.(wakwanza kulia). Wengine ni Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Steven Kebwe, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara, Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Bw. William Erio, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mkulazi Holding, Bw. Ca
NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, NGERENGERE
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu wa Bunge, kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, wamepongeza uamuzi wa Mfuko wa Pensheni wa PPF na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wa kuunganisha nguvu na kuwekeza kwenye mradi wa kiwanda cha sukari, Mkoani Morogoro.
Pongezi hizo walizitoa kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya hadhara na wananchi wa kijiji cha Kidunda, Kata ya Mkulazi, wilaya ya Morogoro mwishoni mwa wiki.
Mawaziri hao ambao walikuwa kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo utakaosimamiwa na kampuni ya Mkulazi Holding, iliyobuniwa na Mifuko hiyo kutekeleza mradi.
“Ninawapongeza, Mfuko wa PPF na NSSF kwa kuitikia mwito wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wenu wa kuunga mkono mipango ya serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda, kwa kuunganisha nguvu na kuwekeza kwenye mradi huu.” Alisema Dkt. Mpango.
Waziri huyo alihimiza taasisi hizo kufanya haraka kukamilisha upembuzi yakinifu, ili utekelezaji kamili wa mradi ufanyike.
Dkt Mpango aliwataka wahandisi kuhakikisha wanatoka maofisini ili kukagua ujenzi wa miundombinu inayoambatana na mradi huo ikiwemo barabara inayojengwa na kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT kuelekea eneo la mradi “Ile barabara ndio itatumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka na kuelekea kiwandani ni vyema kusimamia kikamilifu” alisema Dkt Mpango huku akikisisitiza Kampuni ya SUMA JKT kutekeleza mradi huo kwa kiwango cha ubora ili kulinda imani ya Serikali kwa makampuni ya umma katika utekelezaji wa miradi yake mbalimbali.
Waziri Dkt. Mpango pia aliwapongeza wanakijiji kwa kuupokea mradi kwa ari ya hali ya juu, na kwamba serikali itahakikisha suala la fidia linakamilika kwa haraka ili kuepusha mivutano wakati tayari mradi umekwishakamilika.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, naye aliipongeza Mifuko ya NSSF na PPF kwa uamuzi wake wa kuwekeza kwenye kiwanda hicho ambacho. “Kwa kweli nia ya serikali ni kutengeneza ajira kwa wananchi wetu, naomba watekelezaji wa mradi huu kuanza kuainisha mapema aina ya rasilimali watu watakaohitajika kwenye mradi huu ili serikali ianze kuwaanda vijana wa kitanzania kukamata ajira kwenye kiwanda hiki kikubwa.
Awali Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Steven Kebwe, akizungumza wakati wa mkutano huo aliwashukuru NSSF na PPF kwa kuleta mradi huo katika mkoa wa Morogoro ambapo mradi huo utaenda sambamba na ujenzi wa huduma za kijamii ambapo Dkt Kebwe aliwataka vijana wa eneo hilo kufanya kazi na kuchangamkia mradi unaokuja badala ya kuwategemea wanawake na wazee katika shughuli za uzajishaji.
No comments:
Post a Comment