UZALISHAJI katika kiwanda cha saruji
cha Dangote kilichopo Mtwara umeathirika kwa kiasi kikubwa tokea wiki iliyopita.
Tatizo hili la muda limetokana na hitilafu za kiufundi katika mitambo ya
kiwanda. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Bwana Harpreet Duggal amesema
mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea katika siku
chache zijazo.
Alisema kiwanda kilianza uzalishaji wa
kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine kama hicho jambo
lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo. Hata hivyo alizitaja
hitilafu hizo kuwa ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika kipindi kifupi
kijacho.
Alipoulizwa kuhusu gharama kubwa za
uzalishaji, Bwana Duggal alisema unapolinganisha na gharama nyingine za
uzalishaji katika Dangote, gharama za uendeshaji Tanzania ni za juu mno. Moja
ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda. Na
pia kiwanda kuwepo mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la gharama
za usafirishaji. Akasema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi ya
kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.
Akaongeza, “Tuna matumani makubwa
kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania na tupo makini, kwa
kushirikiana na Serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili tuweze
kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa na
bei nafuu nchini.”
Tangu kuzinduliwa kwa kiwanda cha saruji
cha Dangote, bei ya saruji nchini Tanzania imeshuka kwa zaidi ya asilimia 30.
Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara
chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 600 kina uwekezaji mkubwa katika
saruji kuliko vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo wa kuzalisha tani
milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1000
wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment