October 06, 2016

TRA YAKUSANYA SH TRILIONI 1.37 KWA MWEZI SEPTEMBA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh Trilioni 1.37 katika mwezi Septemba mwaka huu na kufanya jumla ya fedha zilizokusanywa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka mpya wa fedha wa 2016/2017 kufikia sh trilioni 3.59.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo alisema kuwa lengo lililopangwa kukusanywa kwa mwezi Septemba lilikuwa sh Trilioni 1.4.

Kayombo alisema kwa mwaka huu wa fedha TRA imeweka malengo ya kukusanya kiasi cha kodi sh Trilioni 15.1 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali ili kuwezesha kufanikisha malengo ya serikali katika kuhudumia wananchi.

“Mwezi Agpsti tulifamikiwa kukusanya kiasi cha Sh Trilioni 1.13 hivyo mtaweza kuona ni namna gani tumevuka makusanyo ya miezi miwili iliyopita ya Julai na Agosti kwa kufikisha Sh trilioni 1.37,”alisema Kayombo.

 Alisema ukusanyaji wa mapato ya serikali unaenda sambamba na kuelimisha wananchi kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati hivyo.
Wasafirishaji wa mizigo kwenda mikoani wanahimizwa kudai risiti za EFDs pindi wanaponunua bidhaa na kuwa nazo wakati wanasafirisha mizigo ili kuepuka usumbufu pale wanapohitajika kuonyesha risiti hizo. 

Katika hatua nyingine Mamlaka hiyo kuwataka waagizaji wa mizigo nje ya nchi kwa kutumia mfumo wa forodha wa TANCIS kila mara kufuatilia taarifa za upakuaji wa bidhaa zao ili kuepuka udanganyifu wa aina yoyote. 

Kayombo alisema kuwa mfanyabiashara anapotumia mfumo wa TANCIS anaweza kufuatilia mzigo wake kirahisi na kujua hatua zote mzigo wake ulipofikia ikiwa ni ulipaji wa kodi na kila kitu hadi kufika.

“Kwa wale wanaoagiza magari wanashauriwa kupata taarifa za kodi wanayostahili kulipa kabla magari hayajafika ili kuepuka malalamiko ya aina yoyote pale matarajio yao,” alisema Kayombo.

Kuhusu uhakiki wa namba za mlipa kodi (TIN) tayari imehakiki na kutoa vyeti vipya vya TIN 15,467 tangu kuanza kwa kazi hiyo mwezi Agosti mwaka huu.

“Zikiwa zimebaki siku tisa kumaliza zoezi la uhakiki na uboreshaji wa taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kwa mikoa ya kodi ya Dar es salaam na Zanzibar, tayari Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imehakiki na kutoa vyeti vipya vya TIN 15,467,” alisema Kayombo. 

Zoezi la ukakiki na uboreshaji wa taarifa za TIN linaendelea hadi Oktoba 15, mwaka huu katika ofisi za mamlaka hiyo na kuwataka wananchi wenye TIN kujitokeza na kufanya uhakiki kabla muda uliowekwa haujaisha kwani baada ya muda huo kuisha TIN ambayo itakuwa haijahakikiwa itaondolewa katika mfumo wa TIN wa TRA.

No comments:

Post a Comment