October 14, 2016

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU UONDOAJI WA WANANCHI KATIKA MAENEO YALIYOHIFADHIWA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) hivi karibuni Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Angelina Madete na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Eng. Ramo Makani (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawako pichani) Makao Makuu wa Wizara hiyo  Mpingo House hivi karibuni juu ya ufafanuzi wa kuwaondoa wananchi katika maeneo yaliyohifadhiwa. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara Wanyamapori, Prof. Alexander  Songorwa.
_______________________

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Maliasili na Utalii

TAARIFA KWA UMMA

UFAFANUZI KUHUSU UONDOAJI WANANCHI KATIKA MAENEO YALIYOHIFADHIWA

Serikali inawakumbusha wananchi wote na kusisitiza kwamba ni wajibu wao kutii sheria na kuepuka kabisa vitendo viovu vinavyosababisha kupotea kwa uoto wa asili kwa kasi inayoendelea hivi sasa nchini na kutishia UHIFADHI ENDELEVU,  hali hii inapelekea nchi kuwa Jangwa kutokana na ukataji wa miti hovyo, kilimo kisichoendelevu, uchungaji holela wa mifugo, uanzishaji makazi na shughuli zingine za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwa ni pamoja na Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na  Hifadhi za Taifa.

Ikumbukwe kwamba takwimu zinaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania inapoteza takriban hekta 372,000 za uoto wa asili kila mwaka na kwamba kasi hiyo ikiachwa iendelee tishio la kutoweka kwa uoto huo ni kubwa sana. Takwimu pia zinaonyesha kuwa Tanzania ina eneo la uoto wa asili lenye ukubwa wa takriban Hekta milioni 48.1 na kwamba kasi iliyopo ya uharibifu ikiachwa iendelee itaiacha Tanzania bila uoto wa asili baada ya miaka 129.

Takwimu hizi zitabakia hivyo ikiwa idadi ya watu haitaongezeka, ukuaji wa shughuli za kibinadamu hautaongezeka na aina ya shughuli hizo haitabadilika, jambo ambalo haliwezekani. Hivyo basi upo uwezekano wa idadi ya miaka hiyo kupungua hata kufikia nusu, sawa na umri wa kawaida kabisa wa binadamu.

Kutokana na kuzingatia tishio hilo na umuhimu wa uhifadhi katika Taifa kiuchumi, kijamii na kiikolojia, serikali ilitunga sera, sheria, kanuni na Taratibu kwa madhumuni hayo. Sheria hizo ni pamoja na :

·        Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Na. 5 ya mwaka 2009
·        Sheria ya Misitu, Na. 14 ya mwaka 2002
·        Sheria ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Sura 284, R.E 2002
·        Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282, R.E 2002

Kumekuwa na mazoezi yanayoendelea nchini yanayohusu utekelezaji wa sheria hizo ambapo Wakala wa Misitu Tanzania, Taasisi za hifadhi za Wanyamapori n.k zimekuwa zikiendesha mazoezi kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa mbalimbali.

Kufuatia uzoefu katika utekelezaji wa sheria hizi na maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi na wadau wengine, Serikali imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali katika mazingira tofauti na nyakati tofauti kwa kuzingatia sheria husika na kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine:

·        Ongezeko la idadi ya watu na milki zao zinazotokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, dhidi ya ukubwa na ubora wa maeneo yaliyohifadhiwa yanayowazunguka, ikiwa ni pamoja na misitu, mapori ya akiba, mapori tengefu, hifadhi za taifa, njia za mapito ya Wanyamapori (wildlife corridors) na Maeneo ya mtawanyiko wa Wanyamapori (Wildlife dispersal areas) yaliyohifadhiwa kwa miaka mingi.

·        Uvamizi wa maeneo na kuendesha shughuli za kibinadamu kama vile kulima, kuchunga mifugo, kujenga makazi, kuchimba madini, kukata miti hovyo na uvunaji mwingine wa maliasili usiozingatia sheria

·      Kupungua hadhi kwa baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa hata kufikia viwango vya kupoteza sifa zilizosababisha maeneo hayo kuhifadhiwa na hivyo kulisababishia Taifa hasara kubwa kiuchumi, kiikolojia na kijamii

·       Haja ya kuboresha taarifa zinazoendana na wakati na uwiano sahihi kati ya ukubwa na ubora wa ardhi iliyopo katika maeneo na mahitaji halisi ya ardhi (yakiwemo maeneo yaliyohifadhiwa) na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

·       Haja ya kuboresha njia za usimamizi na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kisheria kwa kuzingatia zaidi sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa namna endelevu.

Kwa Taarifa hii, ambayo inatolewa na Wizara ikitekeleza maagizo ya mamlaka za juu za Serikali, inaagizwa kama ifuatavyo:

Kama ilivyoahidi Bungeni na kama ilivyokwishatoa maelezo katika nyakati tofauti, serikali imekwishaunda kikosi kazi chenye wajumbe kutoka Wizara sita zinazohusika moja kwa moja na changamoto mbalimbali za ardhi, kwa madhumuni mapana ya kufanya uchunguzi wa kina na kupitia sheria zote zinazohusika kabla ya kuishauri serikali kuhusu namna bora zaidi na endelevu ya kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo inayohusisha maeneo yaliyohifadhiwa. Kikosi kazi hicho kinatarajiwa kukamilisha kazi yake hivi karibuni.

Katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu na endelevu wa migogoro ya ardhi:

·         Viongozi na Watumishi wanaohusika wasiwabughudhi wananchi na badala yake wazingatie taratibu katika kutekeleza sheria wakati wa kushughulikia ukiukwaji wa sheria kwa wananchi walioko katika vitongoji na vijiji vilivyosajiliwa.

·   Wananchi walioko katika maeneo hayo wasianzishe shughuli mpya za kibinadamu na wasiendelee na shughuli za kibinaadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira na kuathiri tabia nchi

·    Mifugo yote iliyoko ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria iondolewe haraka kwa kuzingatia taratibu

·    Haitarajiwi kwamba Wananchi wengine watatumia vibaya tamko hili na kuanza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa shughuli zozote zile za kibinaadamu kwa kuwa vitendo hivyo havihusiani na tamko hili na hatua kali zitachukuliwa mara moja dhidi ya wale watakaodiriki kwenda kinyume.

Serikali inatarajia kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote wa uhifadhi na wananchi kwa ujumla katika kutekeleza azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi duniani zinazoendana na Malengo ya Dunia (Umoja wa Mataifa), ya Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goals) kupitia uhifadhi endelevu wa maliasili zake.

Wakati Serikali inaendelea kutoa Elimu kwa njia mbalimbali na kufanya uhamasishaji, Wananchi wanatarajiwa pia kujenga na kuimarisha uelewa, utayari na kushiriki katika jitihada hizo za Serikali.


Imetolewa na;

Mhandisi Ramo Makani
Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii

13 Oktoba, 2016

No comments:

Post a Comment