October 16, 2016

CCM WAWALILIA DK MASABURI NA MGODA


Marehemu Dk Didas Masaburi enzi za uhai wake.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na Masikitiko makubwa taarifa za Kifo cha aliyekuwa Meya wa Zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi aliyefarikai Oktoba 12 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa ya Chama hicho imemwelezea Dk Masaburi kuwa alikuwa ni mwanachama mwaminifu wa CCM na kusema kuwa inaungana na familia ya marehemu Masaburi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. 

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg Abdulrahman Kinana ameitumia salamu za rambirambi familia ya Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Iringa Mzee Tasili Mung’wenya Mgoda aliyefariki dunia jana tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Hospitali ya Wilaya ya Mafinga.

Mzee Mgoda amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya TANU baadae CCM na Serikalini ambapo amekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Mafinga, Katibu wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkuu wa Wilaya Mstaafu.

Katika Salamu hizo Ndg Kinana amesema amepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa kifo cha Mzee Tasili Mgoda ambaye alikuwa ni sehemu ya hazina ya wazee wa CCM na kwamba anaungana na familia ya marehemu, ndugu na jamaa katika kipindi hiki kigumu cha huzuni ya kuondokewa na mpendwa wao.

Wana CCM tunamuomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho za Marehemu Mzee Tasili Mung’wenya Mgoda na Dk Didas Masaburi.  Amina

Imetolewa na:-

SELEMAN Y. MWENDA
Kny: MSEMAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
15/10/2016

No comments:

Post a Comment