September 12, 2016

TPB YAISAIDIA SHULE YA MSINGI MBANDE MADAWATI YENYE THAMANI YA SH MILIONI 3.5


Afisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Chichi Banda akiwa katika picha ya pamoja na Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Mbande, Mashaka Mwakyambiki na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya shule hiyo George Anania (kushoto), pamoja na baadhi ya walimu wa shule hiyo na wanafunzi baada ya makabidhiano ya msaada wa madawati 43 yenye thamani ya Milioni 3.5
Wanafunzi wakimsikiliza kwa makini Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mbande, Mashaka Mwakyambikiwakati akitoa neno la shukrani.


Afisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Chichi Banda akiwasihi wanafunzi kusoma kwa bidii katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano ya madawati, kushoto kwake ni Afisa Uhusiano na Mawasiliano ya Benki ya Posta Timotheo Mwakifulefule na kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mbande  Mashaka Mwakyambiki.
Wanafunzi wa shule ya Msingi Mbande iliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam wakifurahia baada ya Benki ya TPB kukabidhi msaada wa madawati 43 yenye thamani ya Milioni 3.5
Afisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Chichi Banda akikata utepe kuashiria kukabidhi ramsi msaada wa madawati 43 yenye thamani ya Milioni 3.5 kwa Shule ya Msingi Mbande. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

 *************
BENKI ya Posta Tanzania (TPB) imetoa msaada wa madawati 43 yenye thamani ya Milioni 3.5 kwa Shule ya msingi Mbande iliyopo kata ya Chamanzi Wilaya ya Temeke.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya madawati hayo mwishoni mwa wiki Ofisa Mawasiliano wa TPB, Chichi Banda, alisema benki hiyo imekuwa ikitoa kipaumbele katika sekta ya elimu kutokana na ukweli usiopingika kuwa elimu ni uti wa mgongo wa taifa lolote hapa duniani.

Alisema madawati hayo yatawasaidia wanafunzi kusoma vizuri pasipo kupata adha yoyote pale wanapokuwa wakimsikiliza Mwalimu pamoja na kuwapuguzia adha ya kukaa chini.

“Msaada huu tuliotoa ni moja ya jitihada za benki yetu katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya kumaliza tatizo la uhaba wa madawati katika shule za msingi” alisema Banda.

Banda alisema benki hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wananchi na kuwa sehemu ya kwanza kuikimbilia ili kutatua changamoto mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka.

Aidha alitoa wito kwa wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii pamoja na walimu kuongeza juhudi katika kuwafundisha ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mashaka Mwakyambiki, aliishukuru benki hiyo kwa kutoa mchango wa madawati ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira mazuri na rafiki.

Alisema hapo awali wanafunzi walikuwa wakisoma wakiwa wamekaa nchini jambo ambalo lilikuwa likisababisha kutokufanya vizuri darasani.

“Tunaishukuru sana TPB kwa kuguswa na ombi letu la upungufu wa madawati na kuamua kutusaidia iliwanafunzi wetu waweze kusoma katika mazingira mazuri” alisema Mwakyambiki.

Mwakyambiki alisema shule hiyo bado ina uhaba wa Madarasa ya kusomea pamoja na uzio na kuomba wadau kujitokeza na kuiga mfano wa TPB.

No comments:

Post a Comment