Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilipatwa na msiba kufuatia ajali ya
basi la Kampuni ya New Force iliyotokea jana tarehe 19 Septemba, 2016 majira ya
saa 2:00 Usiku katika Kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani
Njombe ambapo watu 12 wamepoteza maisha na wengine 28 kujeruhiwa.
Basi hilo limepinduka katika kona ya barabara wakati likisafiri kutoka
Dar es Salaam kwenda Songea Mkoani Ruvuma.
Katika salamu hizo kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema
Nchimbi, Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko
makubwa na kwamba anaungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wote
waliopatwa na msiba katika kipindi kigumu cha majonzi.
"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi naomba
unifikishie pole nyingi kwa wote walipatwa na msiba, wamewapoteza wapendwa wao,
wamewapoteza watu waliowategemea na hakika familia zimetikisika.
"Sote tuwaombee wote waliofikwa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu
na ustahimilivu na pia tuwaombee Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi,
Amina" Amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amewapa pole majeruhi wote na amewaombea wapone
haraka ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila
siku.
No comments:
Post a Comment