September 29, 2016

NEEMA ARORA AELEZEA NAMNA PROGRAMU YA MWANANKE WA WAKATI UJAO ILIVYO MJENGEA UJASIRI

 Neema Arora akiwa ofisini kwake.
 KATIKA kipindi cha miaka mingi iliyopita jamii nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania mfumo dume ulitawala kwa kiasi kikubwa.  Hali hii imechangia  wanawake kubaki nyuma katika nyanja mbalimbali za kijamii.

Chini ya mfumo huu, wanawake wengi wamekosa fursa ya kupata elimu na wachache waliobahatika kupata elimu walikuwa hawaaminiwi kupatiwa nafasi  za kutoa maamuzi ikiwemo uongozi kwa ujumla.

Katika miaka ya karibuni  kumekuwepo  na mabadiliko ambayo taratibu  yameanza kuundoa mfumo dume  ambapo hivi sasa wanawake wameanza kuchomoza na kufanikiwa kupata elimu inayowawezesha kupata nafasi za kufanya kazi za kitaaluma ambazo kwa miaka mingi zilikuwa zikishikiliwa na wanaume pekee ikiwemo kupata fursa za uongozi japo idadi bado ni ndogo kwa kulinganisha na wanaume.

Ili kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma serikali za nchi mbalimbali za Kiafrika ikiwemo Tanzania zimeanza kuhamasisha na kutekeleza mpango wa Elimu kwa Wote ambao kwa kiasi kikubwa umeonyesha kuleta mafanikio pia taasisi zisizo za kiserikali zimeanzisha programu mbalimbali za kuwapatia mafunzo mbalimbali ya kuwajenga uwezo wa kujiamini zaidi.
 Moja ya Programu ambayo imeanzishwa hapa nchini katika miaka ya karibuni kwa ajili ya kuwanoa wanawake wasomi kujifunza masuala ya Utawala na uongozi kwenye bodi za makampuni  inajulikana kama ‘Mwanamke Wa Wakati Ujao’ au kitaalamu kama Female Future Programme. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.

Tangu Programu hii ianzishwe, taasisi  na makampuni mbalimbali  makini ambayo yanazingatia usawa wa kijinsia  tayari yameanza kufadhili wafanyakazi wake wanawake kupata mafunzo yanayotolewa chini ya mpango huu.

Moja ya kampuni ambayo imekuwa       mstari wa mbele kutekeleza mpango wa kuwawezesha wafanyakazi wake  wanawake ambayo imeanza kuwapatia fursa wafanyakazi wake kuhudhuria mafunzo ya Programu ya ‘Mwanamke Wa Wakati Ujao’ ni TBL Group.Kampuni hii pia imekuwa ikitekeleza mpango wa uwezeshaji wanawake ndani ya kampuni ujulikanao kama TBL Women’s Forum (TWF).

Mmoja wa wafanyakazi wa TBL Group,Neema Arora  (pichani chini na Juu) mwenye nafasi ya  Meneja wa upishi wa Bia (Brewing Manager) katika kiwanda cha DarBrew ni miongoni mwa wanafunzi wa kozi ya Female Future Programme.
Katika mahojiano  hivi karibuni alianza kwa kushukuru mwajiri wake kwa kumpatia fursa ya kupata mafunzo yanayotolewa kupitia mpango huu na alieleza kuwa kwa muda  mfupi tangia ajiunge nayo ameweza kujifunza mambo mengi ya utawala ambao hakuyajua kabla pia yamemuongezea kujiamini katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.

Katika Programu  hii alisema wanafundishwa masuala mengi hususani utawala wenye kuleta ufanisi kwa makampuni,kujiaamini na jinsi ya kushiriki na kuchangia mawazo katika vikao vya juu vya bodi za makampuni “Mtaala wa kufundishia unaotumika  ni mzuri na ndani ya kipindi cha  muda mfupi unaweza kumbadilisha mtu kuwa na maarifa na upeo mkubwa na kujiamini.  Jukwaa hili ni fursa pekee kwa Wanawake ambao bado hawapati fursa kubwa za uongozi hususani katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania”,alisema.

Bi.Lilian Machera kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ambaye anairatibu kozi hii alisema inaendeshwa  ATE kwa ushirikiano na taasisi ya Confederation of Norwegian Enterprises ya nchini Norway (NHO)  ambayo dhumuni lake ni kuwapatia wanawake walioajiriwa katika makampuni mbalimbali mafunzo ya uongozi wa juu katika makampuni hayo na kuwajengea uwezo wa kuweza kushiriki katika vikao vya juu vya bodi. Alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo umebainisha kuwa ni wanawake asilimia 35% ndio wanashikilia nafasi za uongozi wakati wanaume wanashikilia asilimia 65%.

Alisema mafunzo haya kwa hapa nchini yanaendeshwa kwa kushirikiana na chuo cha Eastern and Southern African Management Institute  (ESAMI) kilichopo mkoani Arusha na zaidi ni ya vitendo kuliko nadharia “Wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya mpango huu wanaweza kukutana darasani katika siku 14 ndani ya kipindi cha miezi tisa zaidi ya hapo  wanakuwa wanajisomea na kufanya kazi kwa vitendo katika sehemu zao za kazi na wanapofikia mwisho wa mafunzo wanafanya mitihani na kutunukiwa vyeti kwa wale wanaofaulu”.Alisema Machera.

Kwa upande wake Mratibu mwenza wa Programu hii kutoka taasisi ya Confederation of Norwegian Enterprises  (NHO),Mavie Bordvik amesema anafurahi kuona progamu hii imeanzishwa hapa nchini. “Mpango wa mafunzo haya tayari umenufaisha wanawake zaidi ya 200 katika nchi ulipoanzia zikiwemo nchi za Nigeria,Kenya na Uganda.

Alisema  nchi nyingi hususani zinazoendelea mfumo dume umetawala kwa muda mrefu kiasi kwamba kunahitajika jitihada za kuuondoa na kuhakikisha  wanawake wanapata fursa sawa na wanaume au zaidi kwa kuwa wanao uwezo wa kufanya lolote na jinsia yao haiwaondolei uwezo wa kufanya mambo makubwa yanayofanyika hapa duniani ikiwemo kushika nafasi za juu za uongozi na kutoa mawazo na maamuzi magumu.

Bi.Zuhura Muro,mwanamke msomi  aliyebobea katika maswala ya Raslimali Watu na Utawala ambaye amekuwa akishikilia nyadhifa za uongozi  kwenye bodi za makampuni mbalimbali  akiongelea juu ya mpango huu katika mahojiano maalum  alisema “ Mpango wa kuwapatia wanawake mafunzo ya utawala ya Female Future Programme ni moja ya jukwaa la kuwanyanyua wanawake wa Tanzania na kuwafikisha kwenye nafasi za juu za uongozi na kutoa maamuzi”.

Alisema   bado   kuna idadi kubwa ya wanawake wasomi nchini wanaohitaji kujengewa uwezo wa kushika nafasi za juu za uongozi na kushiriki kutoa maamuzi kwenye vikao vya bodi za wakurugenzi wa makampuni na kuna haja ya kuanzishwa mafunzo ya aina haya mengi ili wanawake wengi waweze kufikiwa kwa haraka  na kutoa mchango wao katika kuleta maendeleo kwa taifa.

“Tafiti mbalimbali za kitaalamu zinabainisha wazi kuwa kampuni au taasisi yoyote inayoshirikisha wanawake katika ngazi za  uongozi kwa vyovyote itafanya vizuri na kupata mafanikio kwenye shughuli zake kwa kuwa wanawake ni wepesi wa kujifunza na kutumia ujuzi wao wanaoupata kwa umakini na wanayo dhamira ya kudhihirisha kuwa wanao uwezo wa kufanya mambo makubwa na alishauri wapewe nafasi za juu waonyeshe uwezo wao badala ya kuachwa  nyuma.

“Licha ya changamoto zinazowakabili wanawake katika mzunguko wao wa maisha  ambao wenzao wa jinsia ya kiume hawazipati ni muhimu wapewe fursa kwa kuwa wana uwezo”.

Alimalizia kutoa wito kwa wanawake wote wa Tanzania kuamka na kuchangamkia fursa za kujiendeleza zinapojitokeza na kuachana na mawazo ya kujiona wanyonge mbele ya wanaume.

No comments:

Post a Comment