MABAKI ya ndege yaliyopatikana
katika pwani ya visiwa vya Pemba nchini Tanzania yalitoka kwa ndege ya shirika
la Malaysia Airlines iliyotoweka mwaka 2014, maafisa wa Malaysia
wamethibitisha. Inaripoti BBC.
Waziri wa uchukuzi wa Malaysia
Liow Tiong Lai amesema kupitia taarifa, kwa mujibu wa shirika la habari la
Reuters, kwamba baada ya uchunguzi imebainika kwamba kipande hicho kikubwa cha
bati kilichopatikana mwezi Juni ni cha ndege hiyo safari nambari MH370.
Amesema uamuzi huo ulifikiwa
na wataalamu kutoka Idara ya Usalama wa Safari za Ndege ya Australia (ATSB) na
wale wa kuchunguza usalama wa MH370.
Mapema Julai, waziri wa
uchukuzi wa Australia Darren Chester alikuwa amedokeza kwamba kulikuwa na
uwezekano mkubwa mabaki hayo yalikuwa ya ndege hiyo.
Alisema muundo wa mabaki hayo,
ukubwa wake na muonekano wake viliashiria kwamba yalikuwa ya ndege hiyo ya
Malaysia.
Mabaki hayo pia yalikuwa na
muhuri wa kuonesha tarehe ya kuundwa kwake ambayo ilikuwa Januari 23, 2002. Ndege
hiyo ya Malaysia iliwasilishwa kwa shirika hilo 31 Mei, 2002, kwa mujibu wa
tovuti ya shirika la Channel News Asia.
Awali, wachunguzi walikuwa
wamethibitisha kwamba mabaki yaliyopatikana visiwa vya Reunion mwezi Julai 2015
yalitoka kwa ndege hiyo.
Mabaki mengine yanayodhaniwa
kutoka kwa ndege hiyo yamepatikana Msumbiji, Afrika Kusini na visiwa vya
Rodrigues, Mauritius.
No comments:
Post a Comment