September 24, 2016

DAWASCO WAZINDUA VIZIMBA VYA MAJISAFI MANZESE MPAKANI



Katika kuhakikisha kero ya kukosa Maji inakwisha kwenye maeneo mbalimbali yanayowazunguka wakazi wa jiji la Dar es Salaam, Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es salaam (DAWASCO) imezindua vizimba maalum vya Majisafi katika mitaa mbalimbali ya kata ya Manzese Mpakani iliyopo wilaya ya Kinondoni ili  kuwapunguzia wakazi wa maeneo hayo adhaa ya kutafuta Majisafi na salama kutoka umbali mrefu.

Akizungumza katika uzinduzi huo wa vizimba vya Majisafi, Meneja wa Dawasco mkoa wa Magomeni Mhandisi Pascal Fumbuka ameleeza kuwa wamejenga jumla ya vizimba saba vya Majisafi ambapo mtaa wa mchafu wamejenga vizimba vitatu na katika mtaa wa Muhltani wamejenga vizimba vinne na vizimba hivyo vya Majisafi vinatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya elfu moja wa maeneo hayo.

“Katika kutatua kero ya Maji hapa Manzese mpakani tumejenga vizimba vya Majisafi saba ambapo tunatarajia wakazi zaidi wa elfu moja watanufaika na hivi vizimba vya Majisafi hata hivyo kutokana na ujenzi holela wa makazi ya watu imetuwia ngumu kufikisha bomba kwa kila mkazi ila kwa vizimba vya Majisafi tuamini vitaondoa kabisa kero ya Maji kwani kwa kizimba kimoja tu kina bomba nane na Maji yanapresha kubwa hivyo havitaleta msongamano pamoja usumbufu kwa wakazi pale watakapokuwa wanakinga Maji” alisema Fumbuka.

Kwa upande wa mwenyekiti wa serikali ya mtaa ya Muhltani Bw. Sudy Makamba ameishukuru Dawasco kwa kujenga vizimba hivyo vya Majisafi kwani wakazi wa mtaa wake wamekuwa wakipata adhaa ya kutafuta Majisafi na salama kwa muda mrefu hivyo amewataka wananchi kuvituza pamoja na kulinda miundombinu ya Maji iliyopo katika mtaa wao .

“Nawashukuru sana Dawasco magomeni na uongozi wake kwa kutukumbuka na kujenga vizimba hivi vya Majisafi ambavyo vitasaidia kuondoa kero ya Maji katika mtaa wetu ambao umekuwa haupati Majisafi kwa muda mrefu ila pia natumia fursa hii kuwasihi wakazi wote wa mtaa huu kutuza hivi vizimba pamoja na miundombinu kwani tukiharibu tutarudi katika shida tuliyokuwa nayo mwanzo”  alisema Makamba.

Nae mkazi wa mtaa wa mchafu bi. Martha Faraji amesema kuwa  vizimba hivyo vya Majisafi ni mkombozi mkubwa kwao haswa wanawake ambao wamekuwa wakihangaika na adhaa ya  kukosa majisafi na salama kwa kipindi kirefu ila ameiomba Dawasco kuongeza vizimba hivyo kwenye mtaa wao ilikuepukana na msongamano kwenye vizimba hivyo.

“vizimba hivi vya Majisafi kwa kweli vimetuokoa sisi wanawake wa mtaa wa mchafu maana tulikuwa tunapata shida mno maana tunahangaika kupata majisafi na kwa bei ya juu ambayo sisi watu wakawaida inatuwia ngumu kumudu ila tunaomba Dawasco wajenge vingi ilikusiwe na foleni wakati tunaenda kukinga Maji” alisema Faraji.

No comments:

Post a Comment