Dirisha la usajili kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes na Ligi
Daraja la Pili msimu wa 2016/2017 lilifungwa saa 6.00 usiku wa Jumamosi
Agosti 6, 2016.
Hadi dirisha linafungwa, timu kadhaa
hazikuwasilisha kabisa usajili wake licha ya kukumbushwa kwa njia
mbalimbali na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Usajili wa msimu huu ni kama msimu uliopita kwamba
unafanyika kwa njia au mfumo wa mtandao unaoitwa Transfer Matching
System (TMS) ambao (server) yake au chombo chake cha kutunza kumbukumbu
kipo Makao Makuu ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) -
Uswisi.
Kwa kawaida mfumo huu upo chini ya FIFA na TFF hutoa taarifa kwa FIFA tarehe ya kufungua dirisha la usajili na kufunga.
Mfumo huu uhusisha pande tatu ambazo ni klabu,
shirikisho (TFF) na FIFA. Kimsingi kazi ya usajili hufanywa na klabu
ambako inajaza fomu kwa njia ya mtandao na hupakia viambatanisho kama
vile mikataba ya wachezaji na picha za wachezaji.
Zoezi hili hufanywa na Meneja Usajili wa klabu
husika wakati shirikisho hufanya kazi ya kuhakiki na kuidhinisha tu na
FIFA huratibu na kuusimamia mfumo mzima.
Kabla ya kutangaza kufunguliwa kwa dirisha la
usajili hapo Juni 15, 2016 Shirikisho liliandaa kozi ya mafunzo ya
usajili kwa klabu zote 64 zikiwa ni 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara; 24 zitakazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes na timu 24
zitakazoshiriki Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/2017.
Baadhi ya timu hazikutuma wawakilishi, lakini ziko
zilizofanya jitihada za kuomba usaidizi kwa kufika ofisini TFF kuomba
usaidizi wa kufanya usajili na zilifanikiwa. Kwa Young Africans, licha
ya kuwa hapa Dar es Salaam, haikuomba usaidizi wowote na hata
walipokumbushwa kuhusu suala la usajili, hawakujibu kitu.
Young Africans ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2014/2015 na 2015/2016, ni
moja ya vilabu ambavyo havikutuma mwakilishi kwenye kozi iliyofanyika
Uwanja wa Taifa kwa siku tatu mfululizo ikigusa wawakilishi wa madaraja
ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Meneja wa TMS wa Young Africans ni Katibu Mkuu hakuwahi kupata mafunzo ya TMS.
Hivyo sasa klabu zote ambazo hakuzituma usajili
wake, hazina budi kuandaa utetezi utakaokwenda TFF ambao utatumwa FIFA
yenye mamlaka ya kufungua dirisha, na utetezi huo ukikataliwa timu
husika inabidi ishuke daraja ambalo halimo kwenye usajili wa mfumo wa
TMS.
TFF kwa sasa inasuburi barua ya utetezi wa klabu
ambazo hazikukamilisha zoezi la usajili ili iutume FIFA. Sambamba na
hilo TFF inatathimini mwenendo mzima kisha itatoa taarifa kwa FIFA ili
kuangalia namna gani ya kushughulikia maeneo yaliyokuwa na upungufu kwa
sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment