August 25, 2016

TAZARA YAPONGEZWA KWA UKARABATI WA KICHWA CHA TRENI



Meneja wa TAZARA mkoa wa Tanzania Bw. Fuad Abdallah (kulia), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), wakati alipokuwa akikagua kichwa cha Treni jijini Dar es Salaam.




Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto), akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu (kushoto) namna ya Kichwa cha Treni kinavyofanya kazi wakati alipokuwa akikagua kichwa hicho jijini Dar es Salaam




Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (mwenye suti), akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), mara baada ya kukagua kichwa cha treni ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati katika karakana ya TAZARA mkoani Mbeya. Kushoto kwake ni Meneja wa TAZARA mkoa wa Tanzania Bw. Fuad Abdallah.
************
Serikali imeipongeza Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), kwa kutekeleza agizo la kukamilisha ukarabati wa kichwa cha Treni ndani ya miezi miwili ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati wake  katika karakana ya  Mbeya. 

Akiongea mara baada ya kukikagua kichwa hicho katika karakana ya Mamlaka hiyo jijini Dar es salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwake kutasaidia huduma bora na ya uhakika kwa usafirishaji wa mizigo na abiria.

“Nimefurahishwa na uharaka wenu wa utendaji kazi, kwani nilitoa miezi miwili kwa TAZARA kukarabati  kichwa hiki haraka iwezekanavyo kutokana na umuhimu wake”, amesema Waziri Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa ametoa wito kwa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa moyo na kwa ufanisi ili kuweza kufufua Mamlaka hiyo ambapo kwa kipindi kirefu ilikuwa na misukosuko mingi. 

Naye Meneja wa TAZARA mkoa wa Tanzania Bw. Fuad Abdallah, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mamlaka hiyo itaendelea na huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria ndani na nje ya nchi.

“Kwa sasa TAZARA inaendelea kuboresha na kuimarisha huduma za usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi New Kapiri Mposhi kati ya siku nne hadi saba ukilinganisha na siku zilizopita”, amesema Bw. Fuad.

Kichwa hicho cha Treni kimekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni moja ambapo Serikali imeokoa Bilioni Tisa mpaka Kumi endapo ingenunua kichwa kipya.

No comments:

Post a Comment