August 30, 2016

MKUU WA WILAYA YA ARUSHA AKEMEA UTORO WA MADIWANI

Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro akizungumza na waandishi kukemea hatua ya kuahirishwa Baraza la Madiwani leo kwasababu za kutotimia akidi.
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Gabriel Daqarro amekemea kitendo cha kuahirishwa kikao cha Baraza la Madiwani katika jiji la Arusha kuwa kinawanyima wananchi haki ya kuwakilishwa katika baraza hilo linalojadili maendeleo.

Kikao hicho kimeshindwa kufanyika baada ya madiwani 14 pekee kuhudhuria katika ya madiwani 36 ambao ni wajumbe halali wa kikao hicho.

Meya wa Jiji hilo,Kalist Lazaro amesema amelazimika kuahirisha kikao hicho baada ya akidi kushindwa kutimia huku akidai baadhi ya madiwani wamejificha wakiogopa kukamatwa na polisi kwa kuhamasisha maandamano ya Septemba  Mosi.

Mkuu wa wilaya amepinga kauli hiyo ya Meya na kusema akiwa Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amewasiliana na Mkuu wa polisi wa wilaya(OCD)ambaye alikanusha taarifa za kutafutwa madiwani hao.

Aliwataka madiwani hao  watimize wajibu wao wa kuwawakilisha wananchi waliowachagua badala ya kutoa sababu zisizo na mashiko huku wakifahamu vikao vya baraza la madiwani vipo kisheria na vina gharama kuviandaa.

No comments:

Post a Comment