July 18, 2016

POLISI WATAKIWA KUWAONDOA RAIA KATIKA UTENDAJI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi wote wasiokuwa askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu na uadilifu ndani ya jeshi hilo.

Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016 muda mfupi baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Pamoja na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi kuondolewa katika utumishi wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.

"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.

"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi, kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi la polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi Jeshi la Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na ametaka viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri, wawatie moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama kuwatisha pale wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.

"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo mnaowaongoza mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la IGP liache lishikwe IGP atakwenda kujielezamwenyewe, hata akishika gari la RPC afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa chini wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia liachie, ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba kwelikweli na yule askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli. 

Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo vingine vya serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.

Tukio hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Makatibu Wakuu na Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

No comments:

Post a Comment