Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), Kanda ya Kaskazini Bw. Peter Lusama umuhimu wa kupitisha mkongo wa mawasiliano juu katika eneo la Msamvu linaloathiriwa na mafuriko mara kwa mara mkoani Singida.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitizama kwa karibu mtambo wa kuratibu usalama katika kituo cha kutunza taarifa mbalimbali (data centre) jijini Dar es Salaam. Kituo hicho cha kwanza kujengwa nchini kitatunza taarifa za Serikali na sekta binafsi.BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akitoa maelekezo kwa Meneja
wa Kiwanja cha Ndege mkoani Singida (wa pili kulia), kuhusu mkakati wa Serikali
wa ukarabati na upanuzi wa viwanja vya ndege kumi na moja ikiwemo kiwanja hicho
cha Singida.
Mbunge wa jimbo la Singida
Mjini Mhe. Mussa Sima (wa nne kulia), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), wakati alipokagua
kiwanja cha ndege cha Singida.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akihakiki usahihi wa moja ya kifaa cha kupimia
hali ya hewa katika ofisi za Mamlaka hiyo mkoani Singida. Kushoto ni Meneja wa
Mamlaka ya Hali ya Hewa mkoani Singida Bw. Florian Rweyongeza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Simu
nchini (TTCL), Kanda ya Kaskazini Bw. Peter Lusama(wa tatu kulia), akitoa
taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa
pili kulia), kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mkongo wa taifa mkoani Singida.
*************
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Katibu Mkuu wa Wizara
anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu
nchini (TTCL), kuhakikisha kituo cha kutunzia taarifa (Data Centre) kilichopo
Kijitonyama jijini Dar es Salaam kinaanza kufanya kazi.
Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo
kufuatia kukamilika kwa Data Centre hiyo miezi kadhaa iliyopita na mahitaji ya
wadau wa huduma ya kutunza kumbukumbu za taasisi zao katika kituo hicho
kuongezeka.
“Katibu Mkuu wa Sekta ya
Mawasiliano na Mtendaji mkuu wa TTCL hakikisheni kituo hiki kilichojengwa kwa
gharama kubwa kinaanza kutumika na kuwezesha mashirika na taasisi mbalimbali
kutunza kumbukumbu zao na kuiletea Serikali mapato”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema huduma ya
mtandao katika kituo cha Data Centre imeimarishwa kutokana na kuunganishwa na
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo itawarahisishia wateja wake kuweka na kuchukua
taarifa zao kwa haraka.
Akizungumza mara baada ya kukagua
maeneo mbalimbali unapopita Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Prof. Mbarawa
amemtaka Mkurugenzi wa TTCL kanda ya Kaskazini Bw. Peter Lusama kuhakikisha
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unapitishwa juu ya nyaya katika maeneo yenye changamoto
za mafuriko ili kuepuka uharibifu wa mara kwa mara na usumbufu kwa watumiaji.
Aidha amezitaka taasisi za
Serikali na binafsi kukitumia kituo cha kisasa cha kuhifadhi taarifa DATA
CENTRE kutunza taarifa zao ili kuzihakikishia usalama na uhakika wa kuzitumia
wakati wote, ambapo asilimia 75 imetengwa kwa ajili ya kutunza taarifa kutoka
sekta binafsi na 25 itatunza taarifa za Serikali.
Kituo hicho ambacho ni cha kwanza
kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni fursa mpya kwa
wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi kuzihifadhi na
kuzitumia wanapozihitaji kinamilikiwa na Serikali na ujenzi wake umegharimu
takribani dola za kimarekani milioni 93.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Singida na mahali utakapojengwa uwanja mpya
na kusisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini kusimamia
kikamilifu ujenzi wa uwanja wa ndege wa sasa ambao upembuzi yakinifu wake
umekamilika.
Amesema tayari Serikali
imebainisha viwanja 11 vya ndege nchini kote na kuvifanyia upembuzi yakinifu
kabla ya kuanza kuvijenga ili viweze kukidhi mahitaji ya soko.
Amevitaja viwanja hivyo kuwa ni
Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi, Moshi,
Njombe, Simiyu na Singida ambavyo vitapanuliwa na kujengwa kwa kiwango cha
lami.
No comments:
Post a Comment