Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta
ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka akitoa hotuba ya ufunguzi wa semina ya
siku tano kwa madaktari wanaotoka mikoa ya kanda ya ziwa kuhusu ajali na
magonjwa yanayotokana na kazi Jijini Mwanza. Bi. Isaka alisisitiza umuhimu wa
WCF na madaktari kufanya kazi pamoja ili waweze kulipa fidia stahiki kwa
wafanyakazi wote kutoka sekta Binafsi na Umma. Wengine pichani kutoka kushoto
ni Afisa Utumishi Mkuu, Mkoa wa Mwanza, Bw. Salvatory KyaKyarwenda, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo, Bw. Emmanuel Humba.
********
NA
K-VIS MEDIA, MWANZA
MKURUGENZI
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Bi Irene Isaka
ameipongeza Bodi ya Wadhamini na Mkuurgenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi, (WCF), kwa kuweza kuwafikia wadau
wake muhimu kwanza kabla ya kuanza kutoa Fidia kwa Wafanyakazi.
Bi Isaka aliyasema hayo leo Juni 6, 2016 wakati
akifungua mafunzo ya siku tano kwa madaktari 124 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa
kwenye ukumbi wa jengo la PPF Plaza jijini Mwanza.
Aidha,
amesema kuwa sasa hivi wafanyakazi wasifanye kazi kwa wasiwasi kwani kuna
chombo maalumu ambacho ndiyo kinga na msaada wao endapo watapatwa na majanga
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Pia
Bi. Isaka ametoa wito kwa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), na madaktari kote nchini kufanya kazi
pamoja ili waweze kulipa fidia stahiki kwa wafanyakazi wote kutoka sekta Binafsi
na Umma.
Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, ni taasisi ya
Serikali iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu, na ulianzishwa kwa sheria ya Fidia Kwa
Wafanyakazi namba 20 ya mwaka 2008. Lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha
Mfanyakazi anapata fidia stahiki kutokana na kuumia kazini au magonjwa
yatokanayo na kazi na kwa wanafamilia kupokea fidia kwa niaba ya mwenza wao
aliyefariki akiwa kazini.
Mafao yatolewayo na Mfuko huo ambayo kwa mujibu
wa Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Masha Mshomba ni pamoja na Fao la matibabu, fidia ya
ulemavu wa muda, fidia ya ulemavu wa kudumu, Fidia ya huduma ya marekebisho
(Rehabilitation services), Fedha za uangalizi wa mara zote, (Constant
attendance care grant), Fedha za mazishi, na fidia kwa wategemezi wa
mfanyakazi aliyefariki akiwa kazini au kutokana na maradhi yaliyosababishwa na
kazi aliyokuwa akifanya. “Mfuko utaanza kutoa mafao ya kwanza kabisa tangu
uanzishwe kuanzia mwaka wa fedha unaoanza Julai, 2016/2017.” Alisema Mkurugenzi
Mkuu, Bw. Masha Mshomba.
Mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa WCF na Shirika la Kazi Duniani, ILO.
No comments:
Post a Comment