SHIRIKA la Majisafi na
Majitaka Dar es salaam (DAWASCO), imekanusha taarifa iliyoripotiwa na vyombo
kadhaa vya habari juu ya gari linalodaiwa kuwa la DAWASCO lenye namba za usajili
T 369 BUZ ambalo liliparamia kituo cha mabasi cha Mbuyuni kilichopo maeneo ya Namanga
Oysterbay na kujeruhi watu watatu.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu
Meneja uhusiano wa Dawasco, Bi. Everlasting Lyaro amesema kuwa gari hilo sio
mali ya Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam, bali ni moja ya gari
linalomilikiwa na watu binafsi ambao wanasaidiana na Dawasco katika kusambaza
huduma ya maji maeneo ambayo huduma hiyo bado haijafika kwa kutumia magari
makubwa ya kusambaza Maji (maboza) ambayo yamesajiliwa na kuwekwa nembo ya
Dawasco.
“Gari hili sio mali ya
Dawasco, bali limesajiliwa na Dawasco na kuwekewa viambatanisho vyote muhimu ili kusambaza huduma ya Maji maeneo ambayo
mtandao wa Maji haujafika haujafika,” alisema Lyaro.
Ikumbukwe kuwa mnamo mwezi
Oktoba mwaka jana, Dawasco ilianza zoezi maalum la kusajili visima pamoja na
magari yote makubwa ya kusambaza huduma ya Maji jijini Dar es salaam, ambapo
tayari magari makubwa takribani 256 ya kusambaza huduma ya Maji jijini Dar es
Salaam yamekwisha sajiliwa.
Dawasco inapenda kuvikumbusha
vyombo vya habari kuzingatia taratibu za kazi kwa kuandika taarifa zenye uhakika na ukweli ili
kuepuka upotoshaji wa habari kwa wananchi.
Everlasting Lyaro
Kaimu Meneja
uhusiano- Dawasco
022-2194800 au
08001164
Dawasco Makao
Makuu
30/05/2016
No comments:
Post a Comment