November 01, 2015

ARUSHA KUWA MWENYEJI WA MAJADILIANO YA MASUALA YA KISHERIA BARANI AFRIKA

Na Kulwa Mayombi, EANA
Arusha, 1 Novemba 2015 (EANA)--ZAIDI ya wajumbe 200 wa kada ya sheria kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanatarajia kuhudhuria mkutano wa siku tatu ya majadiliano kuhusu masuala ya sheria barani Afrika unaoanza jumatano  mjini Arusha.

Majadiliano hayo ambayo, yanaratibiwa kwa ushrikiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu wa watu(AfCHPR) yenye makao yake makuu mjini Arusha na Umoja wa Afrika(AU) ,yatawaleta pamoja majaji wakuu wa nchi husika, Marais wa Mahakama za juu na Mahakama za Katiba,wasomi na watendaji wengine wa Mahakama za Kitaifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu,majadiliano hayo ya masuala ya sheria barani Afrika ,ambayo hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili, yana kauli mbiu isemayo 'kuunganisha sheria za kitaifa na zile za kimataifa' ,ni ufuatiliaji wa majadiliano ya kwanza ya aina hiyo yaliyofanyika mjini Arusha mwaka 2013.

"Majadiliano kuhusu sheria barani Afrika yanatoa fursa muhimu ya kubadilishana maarifa kwa lengo la kuanzisha na kukuza ushirikiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na watu kwa upande mmoja na Mahakama za Kikanda na zile za kitaifa kwa upande wa pili" alisema Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na watu,Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Augustino Ramadhani.

Jaji Ramadhani aliongeza kuwa majadiliano hayo pia yatasaidia kukuza masuala ya utawala bora katika sheria na kuhakikisha utoaji bora wa haki kwa wananchi wa nchi za bara la Afrika.

Washiriki katika majadiliano hayo watajadili pamoja na mambo mengine maboresho ya sheria yanayoendelea hivi sasa barani Afrika,hali ilivyo kuhusu sheria za haki za binadamu,utoaji endelevu wa elimu ya sheria,usimamizi wa taasisi za sheria,usimamizi bora wa mifumo ya Mahakama na kubadilishana uzoefu kutoka mabara mengine.

Majadiliano ya kwanza yalizungumzia  kwa ujumla mfumo wa haki za Binadamu barani Afrika na uhusiano baina ya Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu na Tume ya Afrika ya haki za binadamu na watu.

No comments:

Post a Comment