MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA
MAJIMBO
Chama
cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo
kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa
utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa
upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na
Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana
na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba
kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye
sheria.
Kwenye
baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura
kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo
ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa
wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama
kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura.
Hata
hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge,
tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na
tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM
imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu
wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru,
uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni
ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo
ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau
mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na
hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba,
kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo
sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia
malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari
jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa
na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea.
Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo
iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na
sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini
wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu:
Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya
kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo
na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa
tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba
ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa
letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda
na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea
heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku
Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi.
Kwetu
sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na
kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za
ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na
utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea
wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha
katika uchaguzi huu.
Mchakato
wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na
Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada
tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye
mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo.
Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya
Mbozi. Amani ya nchi hii ina thamani
kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya
kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa
kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha,
kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. Tunawaomba Watanzania
waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa
kuilinda amani ya nchi yetu.
January
Makamba
Mjumbe wa
Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015
No comments:
Post a Comment