Afisa Miradi wa kampuni ya Agrics Ltd, Bwana Semeni Kime (wa pili kulia)
akifurahi na wakulima wa kijiji cha Mwakabeya baada ya kuwakabidhi
wakulima hao mbegu za mahindi, alizeti pamoja na mbolea kwa ajili ya
msimu mpya kilimo.
Wakulima wakifurahia mbegu bora za
mahindi, alizeti pamoja na mbolea mara baada ya kukabidhiwa na meneja
miradi kampuni wa kampuni ya Agrics. Wakulima walionufaika na
mbegu hizo ni pamoja na Maswa, Meatu na Shinyanga vijijini.
KAMPUNI ya Agrics imetimiza
ahadi ya kuwakabidhi mbegu bora za mahindi, alizeti na mbolea wakulima wa
Maswa, Meatu na Shinyanga vijijini. Zoezi hili limefanyika kwa wakati kufuatia
msimu mpya wa kilimo kutazamiwa kuanza hivikaribuni. Kampuni ya Agrics iliwapa
fursa wakulima kuchagua aina ya mbegu wazitakazo ili kuhakikisha wanapata kile
wakipendacho.
Wakulima wanaendelea kuandaa
mashamba yao huku wakiwa huru kabisa kwani tayari Agrics imewapatia mbegu zao
kwa mkopo nafuu kabisa na wametanguliza asilimia 25%. Zoezi la kukabidhi mbegu lilisindikizwa na
viongozi mbalimbali wa vijiji ili kuhakikisha wakulima wanajipatia mbegu zao
kwa manufaa ya kijiji na mkoa kwa ujumla.
Akiongea kwa niaba ya Agrics Meneja
miradi Bwana Charles Laswai alisema, “Tunajivunia kuwatimizia watejawetu
mahitaji yao kwa wakati. Kwa sasa wakulima wanasubiri mvua wakiwa na amani
kabisa kwani tayari wana mbegu zao na wapo tayari kuanza kilmo. Kupitia mkopo
wetu wakulima wamejipatia mbegu zao kwa kulipia 25% tu ya mkopo na watalipa asilimia
inayobakia baada ya kuwa wamevuna mazao yao.
Hii ni fursa kubwa kwa mkulima
kwani kwa sasa amepata nafasi nzuri ya kuzingatia kilimo bila kuwaza jinsi ya
kupata pesa ya kulipa. Lengo la Agrics ni kuhakikisha kauli mbiu ya ‘Kilimo
Kwanza’ inazingatiwa na inakuwa ni yenye tija kwa mkulima wa Shinyanga
vijijini, Maswa pamoja na Meatu. ”
“Kwa upande wetu kukabidhi
mbegu kwa mkulima ni mwanzo wa mengi makubwa tutakayomsaidia mkulima katika
msimu huu wa kilimo. Mara zote tumekuwa tukiwajali wateja wetu kwa kushirikiana
na viongozi wa serikali pamoja na wataalamu wa kilimo kuhakikisha tunawapa
mafunzo juu ya kilimo bora na cha kisasa. Elimu hii haiishii tu wakati wakulima
bali hata wakati wa kuvuna na kuhifadhi ili uvunaji na uhifadhi pia uzingatie
teknolojia mpya inayompa fursa mkulima kuvuna mazao yake na kuyahifadhi vizuri
kwa matumizi ya baadae. Tunahakikisha mazao yanahifadhiwa kitaalamu ili yasiathiriwe
na wadudu kwa kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwa wakulima wetu”. Aliongeza Bw. Jonathan
Kifunda, Mkurugenzi wa Agrics Tanzania.
Kampuni ya Agrics huwapatia
wakulima wake mbegu za mahindi aina ya Seedco Tumbili, Seedco Pundamilia,
Pannar na Faru pia huwapatia mbegu za alizeti aina ya Kenyafedha pamoja na
mbolea ya kukuzia aina ya CAN (YARA). Mkulima hujipatia mbegu hizi kwa mkopo
nafuu na hulipa kwa awamu tano ndani ya miezi 9. Mbegu hizi zimedhibitisha
nazinastahimili ukame na wadudu hivyo zinaendana na hali ya hewa ya mikoa ya
Simiyu na Shinyanga na kuwawezesha wakulima kupata mazao mengi zaidi.
“Kampuni ya Agrics imekuwa mkombozi wetu kwa
miaka mingi sasa! Tumekua tukikopeshwa mbegu kwa gharama nafuu kabisa na sasa
wametukabidhi mbegu kwa ajiliya msimu huu kwa wakati, hivyo tuna amani na
tunachosubiri ni mvua zianze kunyesha ili tupande mbegu zetu. Kupitia Agrics
kijiji chetu kina mabadiliko makubwa sana kwani wakulima wengi wameweza kujenga
nyumba za kisasa(kwa vigezo vya nyumba za vijijini) na tuna akiba ya chakula
tofauti na zamani kwani mavuno yalikuwa ni kidogo sana. Binafsi nimeweza
kuwasomesha watoto watatu sekondari na mmoja amejiunga na chuokikuu.Na
nimefanikiwa yote haya kupitia kilimo, suala ambalo lilikuwa ni ndoto kwetu
maana tulitegemea mifugo tu ili tuweze kuwasomesha watoto wetu.” Alieleza bwana
Emmanuel Titus mkazi wa kijiji cha Ipililo wilayani Maswa.
Agrics Ltd ni kampuni ya
kibiashara inayofanya kazi zake kwa kushirikiana na shirika la ICS. Agrics
inawapa wakulima wadogo wa kanda ya ziwa nchini Tanzania na Kenya fursa ya
kujipatia mbegu bora na za kisasa kwa mkopo nafuu unaolipwa kwa awamu zinazompa
mkulima nafasi nzuri ya kujiendeleza. Pia Agrics inahakikisha akiba ya chakula
kwa mkulima ni lazima kwa ajili ya kupunguza njaa kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment