Aisha Madinda enzi za uhai wake
TASNIA ya sanaa imezidi kupata majozi baada ya aliyekuwa mnenguaji wa
bendi za African Stars 'Twanga Pepeta' na Extra Bongo, Aisha Mohammed
Mbegu 'Aisha Madinda' amefariki dunia mchana huu akiwa ndani ya Bajaj
wakati akiwahi hospitali ya Mwananyamala.
Taarifa ambazo blog hii imezipata zinasema kuwa Aisha Madinda alikodisha Bajaj na wakiwa kwenye foleni alikumbwa na mauti na mwili wake kwa sasa upo hospitali ya Mwananyamala ukiwa umehifadhiwa.
Akiongea na EATV Mkurugenzi wa bendi ya Twanga Pepeta amesema kuwa alipewa taarifa na daktari mmoja kuwa wameona kama mwili wa Aisha Madinda hospitalini hapo, ndipo akatuma watu kwenda kuangalia akiwemo Luiza Mbutu ili kuhakikisha kama kweli ni yeye ndipo walipogundua ni yeye.
“Mimi nipo njiani natoka Kigoma kuja Dar es Salaam, ni habari ya kusikitisha sana maana Aisha amefariki katika mazingira ya kutatanisha sana, jana alikuwa mzima na anachati na watu kwenye simu leo napigiwa simu mwili wake umekutwa umehifadhiwa kwenye hospitali ya Mwananyamala, hata sielewi nini kimetokea,” amesema Asha Baraka.
Hata hivyo taarifa ambazo hazijathibitishwa zinadai kuwa Madinda aliita dereva wa bajaj na kuomba apelekwe Mwananyamala Hospitali na kukumbwa na mauti njiani bila dereva kujua mpaka akiwa hospitalini hapo.
Inaelezwa kuwa msiba wa marehemu Aisha uko Kigamboni na huenda akazikwa kesho huko huko.
Aisha madinda atakumbukwa kwa staili yake ya kushambulia jukwaa na kifo chake kimekuja siku moja tu baada ya nguli mwingine wa muziki wa dansi nchini, Shem Karenga kuzikwa.
No comments:
Post a Comment