March 25, 2013

TAARIFA ZA SOKA TOKA TFF HII LEO

MECHI YA TAIFA STARS YAINGIZA MIL 226/-
Mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia  kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jana (Machi 24 mwaka huu) na Stars kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 imeingiza sh. 226,546,000.

Fedha hizo zimepatikana kutokana na watazamaji 32,614 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.

Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 34,557,864.41, maandalizi ya mchezo sh. 28,450,000 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 8,625,641.88.

Nyingine ni bonasi kwa timu ya Taifa Stars sh. 28,798,220.34, asilimia 15 ya uwanja sh. 18,917,141.01, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 25,222,854.67 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 6,305,713.67.

Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 71,885,135.82 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,783,428.20 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.


TENGA AWAPONGEZA WACHEZAJI, SERIKALI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameipongeza wachezaji wa Taifa Stars na benchi lao la ufundi, washabiki, mdhamini na Serikali kwa kufanikisha ushindi wa jana.

Tenga amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano kutoka kwa wadau wote, na hasa wachezaji walioonesha kiwango kikubwa kulinganisha na mechi zilizopita ikiwemo kiwango cha kujituma uwanjani.

Amesema Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu katika miundombinu, usalama na idara zake mbalimbali ikiwemo Uhamiaji ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa mechi hiyo ambapo Taifa Stars iliifunga Morocco mabao 3-1.

TENGA KUFUNGUA SEMINA ELEKEZI COPA COCA COLA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina elekezi ya michuano ya Copa Coca Cola itakayofanyika kesho (Machi 26 mwaka huu).

Semina hiyo inayoshirikisha makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na itafunguliwa na Rais Tenga kuanzia saa 3 kamili asubuhi.

Washiriki wengine katika semina hiyo itakayokuwa na watoa mada kutoka TFF na wadhamini kampuni ya Coca Cola ni waratibu wa michuano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).

No comments:

Post a Comment