December 01, 2012

NGASA AFUNGA GOLI 5 KILI STARS IKISHINDA 7-0 DHIDI YA SOMALIA



Kikosi cha Kilimanjaro Stars kilichopambana na timu ay Somalia katika mchezo wa michuano ya Tusker Cecafa Challenge Cup uliofanyika katika Uwanja wa Lugogo nchini Uganda leo na kushinda kwa goli 7-0. Magoli ya Kilimanjarto Star yakipachikwa na Mrisho Ngasa (5) na John Boko (2).
Mrisho Ngassa akishangilia moja ya goli kati ya matano aliyofunga wakati wa mchezo na Somalia uliochezwa katika Uwanja wa Lugogo nchini Uganda.
 Mlizni Erasto Nyoni akijaribu kumdhibiti Mshambuliaji wa timu ya Somalia asilete madhara.
Boko akishangilia moja ya goli wakati wa mchezo na Somailia
Mashabiki wa timu ya Kilimanjaro Stars waishio nchini uganda wakiishangilia timu yao wakati mchezo dhidi ya timu ya Somalia
 ******
Na Mwandishi wetu, Kampala
TIMU ya Soka ya TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imefuzu kuingia Robo Fainali ya michuano ya Tusker  CECAFA Challenge, baada ya kuilaza Somalia mabao 7-0 katika mchezo   uliopigwa Uwanja wa Lugogo mjini hapa.

Matokeo hayo yanaifanya Bara itimize pointi sita baada ya kucheza mechi tatu huku wakishinda mbili na kufungwa moja tu.

Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager leo ilionyesha kandanda safi na kusisimua mashabiki wa Tanzania waliokuja kuiunga mkono hapa, akiwemo Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Alhaj Juma Nkamia.

Iliwachukua sekunde 48 tu Stars kupata bao la kwanza, kupitia kwa mshambuliaji wa Simba SC, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premum Lager pia, Mrisho Khlfan Ngassa aliyewazidi ujanja mabeki wa Somalia.

Kabla hawajakaa vizuri, Somalia walipachikwa bao la pili, dakika ya 23 lililofungwa na Ngassa tena, aliyeunganisha kona nzuri ya Issa Rashid.

John Bocco ‘Adebayor’ alifunga bao la tatu katika mchezo wa leo na la tatu kwake katika mashindano haya dakika ya 26 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Issa Rashid kutoka wingi ya kushoto.

Bocco tena aliwainua vitini mashabiki wa Tanzania kwa kufunga bao la nne kwa kichwa, akiunganisha krosi ya Ngassa dakika ya 41.

Ngassa alifunga bao la tatu katika mchezo wa leo dakika ya 44 na la tano kwa Stars baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Hussein Abdallah kufuatia shuti kali la Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’

Somalia ilipata pigo dakika ya 30, baada ya kipa wake namba moja, Mohamed Abdullah kuumia baada ya kugongana na Bocco na kutoka, nafasi yake ikichukuliwa na Hussein Abdallah.

Katika kipindi cha pili Ngassa aliendeleza mvua yake ya mabao na kufunga mabao mawili zaidi moja dakika ya 73 na lingine dakika ya 74  hivi kumfanya awe amefunga mabao tano mpaka sasa.

Kocha wa Stars, Mdenmark Kim Pouslen baada ya mchezo huo, alisema huu ni ushindi muhimu kwa kikosi chake kwani sasa watacheza robo fainali.

“Vijana wamecheza vizuri kabisa na kuzingatia kuwa mechi hii ilikuwa muhimu kwao na tumeibuka na ushindi mnono wa mabao saba,” alisema.

Mbunge Nkamia alisema kwamba amevutiwa na soka ya vijana leo na anaamini wana uwezo wa kurejea na Kombe nyumbani. Nkamia aliwapongeza wadhamini wa Stars, Kilimanjaro Premium Lager kwa kuchangia mafanikio ya timu hiyo tangu waanze kuidhamini na akaomba Watanzania zaidi wajitokeze mjini hapa kuisapiti timu hiyo.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe ametuma salamu za pongezi kwa ushindi wa leo na mafanikio ya kutinga Robo Fainali na kusema wao wana imani kuwa Stars itarejea nyumbani na kombe hili.

“Tuna imani kubwa vijana wataendelea kufanya vizuri, kikubwa tu tuwape sapoti kama watanzania ili wasonge mbele zaidi,” alisema.

Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kevin Yondan, Shaaban Nditi, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Frank Domayo na Amri Kiemba.

Somalia; Mohalim Abdullahi/Hussein Abdallah dk30, Ali Mohamed, Said Mahamud, Ali Dadir, Sadaq Abdikadir, Mohamed Salah, Abdikarim Abubakar, Abdallah Mohamed/Hamza Mukhtar, Ahmed Abdikadir Dahir/Muhad Hajji na Ali Ahmed Ali.  

No comments:

Post a Comment