December 28, 2012

ABWAO ALIA NA HALMASHAURI KUMTUMIA KABATI KUGAWA MIKOPO IRINGA

UAMUZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kumtumia Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Rita Kabati (Pichani kulia)(CCM) kugawa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali umemkasirisha Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Iringa, Chiku Abwao (pichani kushoto) (Chadema).
Katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini hapa, Abwao alisema haikuwa sahihi kwa Manispaa hiyo kutoa fursa hiyo kwa Kabati kwa kuwa anaitumia kisiasa.
Mikopo hiyo yenye thamani ya Sh Milioni 10.8 ilitolewa hivi karibuni kwa vikundi 11 vya wanawake na vijana wajasiriamali wa mjini hapa.
“Si haki pesa za halmashauri zikatumika kuwabeba wanasiasa, Kabati amepewa fursa hiyo na amekuwa akitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwamba mikopo hiyo ametoa yeye,” alisema katika kikao hicho ambacho Kabati hakuhudhuria.
Akiomba radhi, Mkurugenzi wa Halmshauri ya Manispaa hiyo, Theresia Mahongo alisema halmashauri hiyo haikuwa na nia ya yoyote ya kisiasa wakati ikitoa mikopo hiyo.
“Huu ni utaratibu wa kawaida wa kuwateua wageni rasmi tunapokuwa na shughuli mbalimbali, wakati tukitoa mikopo hiyo fursa hiyi tulimpa Kabati na hatukuona kama inaweza kuwa na tafsiri hiyo ya kisiasa,” alisema.
 
Alisema kwa kuwa halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo kama hiyo, fursa hiyo itaendelea kutolewa kwa viongozi wengine pasipo kuzingatia itikadi zao kisiasa.
Pamoja na kutoa utetezi huo, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema hakuwa na taarifa ya halmashauri hiyo kutoa mikopo hiyo.
“Hatuhitaji kusigana na watendaji wa halmashauri, ila mnao wajibu wa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni wakati mnatekeleza wajibu wenu,” alisema.
Alisema tangu awe mbunge wa jimbo hilo, idara pekee ambayo imekuwa ikitoa taarifa za utendaji kwake ni ya Ujenzi na anashangazwa kwanini idara zingine hazimpi taarifa wakati wahusika wake wanajua kwamba yeye ni mwakilishi wa wananchi.
Hoja ya Mchungaji Msigwa ilipingwa vikali na Diwani wa Kata ya Ruaha, Alphonce Mlagala aliyesema mbunge kama mwakilishi wa wananchi ana wajibu wa kufuatilia na kuuliza shughuli mbalimbali zinazofanywa na halmshauri.
“Yeye kama mwakilishi wa wananchi na kama tulivyo sisi, hapaswi kusibiri apelekewe taarifa ofisini kwake, anatakiwa kufuatilia kwasababu kazi anayofanya ni ya wananchi,” alisema.
Akijibu hoja ya Diwani huyo, Mchungaji Msigwa alisema yeye kama mbunge ana majukumu mengi ikiwemo kuhudhuria vikao vya bunge kwahiyo ni muhimu kwa halmshauri hiyo ikawa inatoa taarifa za shughuli mbalimbali zinazofanywa bila kujali kama yupo au hayupo.
Kikao hicho kilichopitia taarifa za kamati mbalimbali za halmshauri hiyo, kimeahirishwa mpaka Januari 14, mwakani.

No comments:

Post a Comment