Na Mwandishi wa EANA
Waziri wa Biashara wa Sweden, Ewa Bjorling amewapa changamoto
wafanyabiashara na wanawake nchini mwake kutumia nafasi nyingi zilizopo
kuwekeza katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Akihutubia umati mkubwa mjini Stockholm, Sweden hivi
karibuni,kwenye Jukwaaa la Kwanza la Wanyabiashara wa Sweden na EAC, Waziri
huyo alisema kwamba uwekezaji unakua kwa haraka katika kanda hiyo na kusisitiza
kwamba kanda hiyo ina mazingira bora ya kuweza kufanya biashara.
‘’Kanda ina nafasi lukuki katika sekta za madini,
utengenezaji bidhaa, afya, kilimo na huduma
za teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT),miongoni mwa nafasi zilizopo,’’
aliuambia mkutano huo na kuongeza kwamba Afrika hivi sasa inakuja juu kwa maswala
ya uwekezaji na imejipanga kuwa katika hali nzuri zaidi kiuchumi siku za usoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya EAC na
nakala yake kupatikana kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA),
Waziri Bjorling alieleza kwamba EAC imeonyesha uwezo wa kufanya mabadiliko,
kukuza uchumi na kuleta maendeleo.
Naye Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera kwa upande wake
alisema kwamba, wakati kanda ya EAC inatafuta wawekeaji, wafanyabiashara wa
kanda hiyo pia hawana budi kusaka nasafu zinazopatikana nchini Sweden.
‘’Raia wa EAC nao wanahitaji kuzisaka nafasi za kuwekeza
zinazotolewa na Sweden.Ninaamini kwamba hatua hiyo itatoa nafasi muafaka baina
ya pande zote mbili kuimarisha uchumi,’’ alisisitiza.
Katibu Mkuu pia alikaribisha majadiliano baina ya Chama cha
Wafanyabishara cha Sweden na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara wa Afrika
Mashariki kwa lengo la kuhamasisha ujuzi kwa wanawake ili kuunganisha nafasi za
biashara baina ya pande hizo mbili.
Mapema Kiongozi wa Mabalozi wa EAC nchini Sweden kutoka
nchini Uganda, Joseph Tomusange alisema kuwa EAC ni eneo lenye amani na ni
salama kwa uwekezaji.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi wa mawakala wa
uwekezaji kutoka nchi wananchama wa EAC ambao walitoa maelezo juu ya nafasi za
uwkezaji zilizopo na manufaa yake.
No comments:
Post a Comment