Na Issac Mwangi, EANA
Arusha, Novemba 24,2012 (EANA)
– Masuala ya hali tete ya usalama yanaweza kuleta athari katika uchaguzi mkuu
ujao nchini Kenya, Timu ya Tathmini ya Awali ya uchaguzi huo toka Jumuaiya ya
Afrika Mashariki (EAC) imetahadharisha.
Kufuatia mwaliko wa kufanya
tathmini ya awali ya uchaguzi huo, uliotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi ya
Kenya(IEBC), taarifa ya timu hiyo iliyonaswa na Shirika Huru la Habari la
Afrika Mashariki (EANA) imeleza :‘’Suala la Baraza la Jamhuri ya
Mombasa,mgogoro wa Tana River, Kisumu na Baragoi’’linahitaji kudhibitiwa ili
kutoathiri ushiriki wa raia katika uchaguzi huo.
‘’Kamati ya usalama ya
uchaguzi (Kamati za Usalama za Kitaifa, mikoa na wilaya) kwa kushirikiana na
wakala nyingine za serikali zina nafasi muhimu katika jambo hili ili
kuhamasisha uchaguzi kuwa wa amani,’’ ilieleza taarifa hiyo.
Timu hiyo ya EAC inayoongozwa
na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Dk. Bandru Kiggundu, imejumuisha
wajumbe 30 kutoka kwenye tume za uchaguzi za taifa kutoka nchi wanachama, Bunge
la Afrika Mashariki (EALA) na Sekretarieti ya EAC.
Wawakilishi kutoka Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Taasisi ya Uchaguzi na Demokrasia Endelevu Barani
Afrika walishiriki pia katika utaratibu wa ushirikiano baina ya taasisi hizo na
EAC.
Lengo la msingi la kufanya
tathmini ya awali kati ya Novemba 15 na 16, mwaka huu ni kuhakiki hali ya
utayari wa IEBC, vyama vya siasa, vyama vya kiraia na wadau wengine muhimu
katika mwenendo mzima wa maandalizi ya uchaguzi.
Matokeo ya tathmini ya timu
hiyo yanalenga kupelekwa kwa timu za EAC za uangalizi wa uchaguzi huo za muda
mrefu na muda mfupi.
Pamoja na mambo mengine timu
hiyo ya EAC imebaini kuwepo kwa maendeleo katika sheria za uchaguzi lakini
imetoa wito wa kuwepo kwa utashi wa kisiasa ili kuwezesha sheria zilizopo kutoa
utatuzi wa migogoro inayotokana na uchaguzi.
Huku timu hiyo ikipongeza
‘’mabadiliko ya kisheria’’yaliokwishafanyika, timu pia imetoa wito wa kutungwa
kwa sheria za masuala ya uchaguzi zilizosalia kama vile sheria ya Fedha za
Kampeni, ambayo timu hiyo inasema itatoa uwazi zaidi na usawa katika uchaguzi.
No comments:
Post a Comment