Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Aprili 2 mwaka huu) kupitia ripoti mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza umezingatia Kanuni ya 25(f) ya Ligi Kuu ya Vodacom juu ya Udhibiti wa Wachezaji.
Kanuni hiyo inasema: “Ni lazima kwa klabu na wachezaji kutunza kumbukumbu za kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na mabao matatu (3), iwapo mchezaji atacheza akiwa haruhusiwi kucheza kwa ajili ya kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo. Endapo klabu haina uhakika au inataka taarifa ya idadi ya kadi zake itaomba kwa maandishi toka TFF.”
Cannavaro alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga kwenye mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi hiyo anastahili kukosa mechi tatu. Mchezaji amekosa mechi mbili tu.
Pia klabu za Coastal Union na Yanga zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wake kutupa chupa za majini uwanjani wakati wa mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).
Kamati ya Ligi pia imemuondoa Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kwenye orodha ya waamuzi kutokana na upungufu uliopo kwenye ripoti yake ambapo baadhi ya matukio makubwa hakuyaripoti. Moja ya matukio hayo ni kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo kuzozana na mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza.
Vilevile waamuzi wa mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba wameandikiwa barua ya onyo kwa kupata alama za chini. Waamuzi hao ni Hashim Abdallah, Abdallah Selega, Hamis Chang’walu na Hassan Mwinchum. Naye Kamishna wa mechi namba 153 kati ya Moro United na Villa Squad, Arthur Mambeta amepewa onyo kutokana na upungufu katika ripoti yake.
TFF YAPONGEZA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewapongeza waandishi watatu wa habari za michezo kwa kushinda tuzo ya uandishi bora ya EJAT inayotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Waandishi hao walioshinda katika kategori ya mpira wa miguu ni Imani Mani wa Daily News (magazeti), Abdallah Majura wa 91.2 Sport FM (redio) na Anuary Mkama wa Mlimani Media (televisheni).
TFF inawapongeza waandishi hao kwa ushindi huo uliotokana na makala zao ambazo zina mchango katika maendeleo ya mpira wa miguu, lakini pia ni changamoto kwa waandishi wengine ambao hawakufanikiwa kushinda.
Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika ustawi wa mpira wa miguu, kwani katika nchi nyingine vimefichua rushwa katika mpira wa miguu. Ni matarajio yetu kuwa vyombo vya habari nchini navyo vitakuwa mstari wa mbele katika kufichua na kupambana na rushwa katika mpira wa miguu nchini.
TWIGA STARS YASAIDIWA JEZI ZA MAZOEZI
Kampuni ya Galileo by Travelport Tanzania imetoa msaada wa jezi za mazoezi na maji kwa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) wenye thamani sh. milioni 1.5.
Msaada huo umekabidhiwa leo (Aprili 3 mwaka huu) na Meneja Biashara wa Galileo by Travelport Tanzania, Margret Leslie ambaye amesema wameitikia mwito wa kuisadia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali inayoikabili.
TFF imeishukuru kampuni hiyo ya uwakala wa tiketi za ndege kwa msaada huo na kuzitaka kampuni, taasisi na watu binafsi kujitokeza kuisaidia Twiga Stars ambayo kwa sasa haina mdhamini, kwani gharama za mashindano ni kubwa.
No comments:
Post a Comment