December 05, 2011

Udanganyifu wa Serikali kupitia TOVUTI YA WANANCHI

Jamani Wananchi wenzangu naomba kuwauliza iwapo Tovuti hii ni mali ya Serikali kweli na je iliandaliwa maalum kwaajili ya wananchi kutoa maoni yao au ndio miongoni mwa zile huduma hewa za setrikali kwa wananchi ?.

Binafsi nilipoona kuwa ni tovuti ya serikali kwaajili ya kutoa maoni na kuwasilisha hoja na kero mbalimbali za wananchi kwaserikali na taasisi zake nilifarijika sana kuwa kumbe mwananchi wa kule Kinyenze Wilaya ya Mvomero ambaye amebahatika kupata simu ya mchina iliyounganishwa na Mtandao wa Intanenti anaweza kutuma maoni yake lakini yasipatiwe majibu zaidi ya miezi 6  inauma sana.
Hakika serikali kupitia TOVUTI YA WANANCHI inatudanganya na kudhihirisha wazi utendaji na utoaji mbovu wa huduma za jamii. Leo utalalamikiaje Huduma mbovu za Hosoitali ambayo haina madawa wala madaktari ilhali tovuti tu Serikali imeshindwa kuiendesha.

Lakini Kumbe tovuti hii haiwezi kumsaidia Mlalahoi yule ambaye hawezi kufika mjini kuonana na DC/RC au hata Waziri bila kuweka miadi ya takribani wiki na siku hiyo ahakikishe ana nguo mpya au kiatu kipya kwaajili ya kupenya kw Katibu Muktasi ili amuone huyo.

Inashangaza sana kuona Mwananchi aliyetuma hoja yake Juni 1, 2011 hadi hii leo akiuliza majibu anaambiwa Hoja yako bado haijapatiwa majibu. Dah! Inamaana kama mtu huyu angeamua kufika moja kwa moja ofisi husika si ndo kela siku angeambiwa njoo kesho nenda rudi hadi hiyo nguo yake mpya na kiatu vinachakalia njiani?

Idara ya Habari MAELEZO ninyi ndio mnahusika moja kwa moja na Tovuti hii ya kuwadanganyia wananchi, nadhani mliagizwa kuitengeneza ili kupunguza msururu wa wananchi (Wapigakura) wanaojaa katika maofisi kulalamika huduma mbovu na manyanyaso wanayoyapata huko mtaani kama wale wa Kinyenze ambao wamenyanganywa mashamba yao na hawana pakulima hadi hii leo na hoja yao waliamua kuifikisha kwa mtandao wenu mnaouita Tovuti ya wananchi na wasipate majibu hadi leo huku misimu ya kilimo ikikatika.

MAELEZO mkikwepa basi lawama ziwaendee Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo (kama ilivyoandikwa katika tovuti hiyo. Wizara ya Kutuhabarisha sasa mnatudanganya jamani. Au tumtupie nani zigo hili la misumari alibebe? Eti Mheshimiwa Dakitari mara mbili, Nchimbi na Dokita mwenzako Fenela mnahusika na hili au ndo ilikuwa zuga ya kutupunguza wakulia lia maofisini kwenu?.

TOVUTI YA WANANCHI (www.wananchi.go.tz)   naweza kusema ni moja ya ile miradi iliyoigharimu serikali Fedha za sisi walipa Kodi na wazulumiwa huku vijijini Ambao huishia katika Makabrasha na Shelfu za Maofisi mengi ya Serikali bila Utekelezaji yakinifu licha ya wahusika kukaa semina, mikutano na makongamano na hata kufanya uzinduzi na mwisho ndio kama hivi.

Pia yeyote aliye na majibu ya utendaji kazi wa tovuti hii inayo pokea maoni ya wananchi bila kuyafanyia kazi atujuze kupitia Blogu hii ya Wananchi.

Binafsisheni hii tovuti kama mmeshindwa kuiendesha kama ambavyo Vyoo vyote mijini vimebinafsishwa baada ya serikali kushindwa kuviendesha na leo tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.


No comments:

Post a Comment