Nafasi Ya Matangazo

May 10, 2024

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akikagua eneo ambalo lilifanyika zoezi la kufukuza tembo kuwarudisha hifadhini katika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.
Baadhi ya tembo walioondolewa katika maeneo ya wananchi na kurudishwa hifadhini Wilayani Mbarali, Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa zoezi la  kuondoa tembo kwenye maeneo ya wananchi, Wilaya uya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa zoezi la  kuondoa tembo kwenye maeneo ya wananchi, Wilaya uya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii  imedhamiria kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori  huku ikisisitiza kuwa  katika bajeti  ya mwaka wa fedha  2024/2025 imeweka kipaumbele  katika kutatua changamoto hiyo.
 
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) wakati wa zoezi la kuwarudisha tembo hifadhini lililofanyika Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya leo Mei 9,2024.
 
"Tumefanikiwa kuwarudisha hifadhini tembo takriban 61 na leo tumefukuza tembo 18" Mhe. Kairuki amesisitiza.
 
Amesema hiyo inathibitisha umakini wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujali usalama wa maisha  ya wananchi  na mali zao na uhifadhi  wa rasilimali  za wanyamapori na misitu.
 
Waziri Kairuki amesisitiza kuwa Serikali itafanya kila liwezekanalo kutatua  changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususan  tembo, Simba  fisi madoa, chui, mamba, kiboko, nyani na tumbili.
 
"Tutaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa kila aina ya wanyama na mikakati ya wanyama husika" amesisitiza.
 
Amesema  zoezi hilo la kufukuza tembo kwa kutumia helikopta limeambatana na kufunga mikanda ya mawasiliano kwa tembo viongozi  wa makundi mbalimbali ambapo mpaka sasa imeshafungwa mikanda miwili lakini zoezi litamalizia kwa mkanda wa tatu.
 
Pia, amesema  Rais Samia ameelekeza kwamba wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu walipwe kifuta jasho/machozi katika vijiji vya  Igunda , Rujewa, Mapogoro, Mlungu, lwalanje,Vikaye, Nyeregete, Manyenga na Mwanavala.
 
Aidha, Mhe. Kairuki amezielekeza Taasisi za TANAPA, TAWA na TFS kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi mazingira na namna ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi yao.
 
Mkutano huo umehudhuriwa na Watendaji, Maafisa Waandamizi  na Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii,TAWA, TAWIRI, TANAPA, TFS, viongozi wa Chama  pamoja na wananchi.

Posted by MROKI On Friday, May 10, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo