Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akijibu swali la Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole bungeni jijini Dodoma aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa Kituo cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.
************
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.
Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya umeme itakayoboresha upatikanaji umeme mkoani Songwe ikiwemo ujenzi wa kituo
cha umeme na _switching station_ .
Naibu Waziri Kapinga amesema
hayo tarehe 8 Mei, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la
Mbunge Mbozi, Mhe. George Mwenisongole aliyetaka kufahamu ni lini ujenzi wa
Kituo cha upoza Umeme Kakozi, Tunduma utaanza.
Akijibu swali hilo Mhe.
Kapinga alisema "Serikali kupitia mradi wa TAZA unaotekelezwa na TANESCO
ipo katika hatua za awali za ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nkangamo
(Tunduma) kilichopo takribani kilomita 28 kutoka Kijiji cha Kakozi, Mbozi.
Ujenzi wa kituo hiki unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo kwa sasa
mkataba kati ya TANESCO na mkandarasi atakayejenga kituo hiki tayari
umeshasainiwa."
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa
kituo hicho cha Nkangamo (Tunduma) kutawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika
katika Kijiji cha Kakozi na maeneo mengine ya Jimbo la Mbozi.
Akizungumzia hali ya
upatikanaji umeme kwa ujumla mkoani Songwe, Kapinga amesema kuwa mkoa huo
unapata umeme kutoka kituo cha Mwakibete kilichopo mkoani Mbeya ambapo laini
hiyo ya umeme ni ndefu sana na kupelekea kutokea kwa changamoto za upatikanaji
umeme mkoani Songwe.
Kutokana na hilo amesema
Serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo ya kujengwa switching station
mkoani Songwe pamoja na kituo cha umeme kitakachojengwa kupitia mradi wa
TAZA huku uboreshaji wa miundombinu ya umeme ukiendelea.
Akijibu swali la Mbunge wa
Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kufahamu ni lini kituo cha umeme cha
Uhuru kitakamilika, Mhe. Kapinga amesema kituo kipo ukingoni
kukamilika na hivyo kuboresha hali ya umeme wilayani Urambo.
0 comments:
Post a Comment