Nafasi Ya Matangazo

April 14, 2024

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.Dkt. Selemani Jafo, baada ya kutembelea baanda la maonesho la Ofisi hiyo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Nyamazi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akikagua banda la Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi leo Aprili 14, 2024. Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa Serikali alipowasili katika viwanja vya Nyamazi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, kwa ajili ya Uzinduzi Rasmin wa  Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa  Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika leo 14-4-2024 katika viwanja hivyo.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi , wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, wakati akitembelea banda la maoneshe la Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya maonesho vya Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, wakimsikiliza Afisa Masoko na Uhusiano wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) Asha Kassim Biwii,wakati akitembelea banda la maoneshe la (ZHSF) wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya maonesho vya Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 14-4-2024.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, akimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Fatma Mabrouk Khamis ,wakati akitembelea banda la maonesho la Wizara hiyo katika viwanja vya Maonesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B”, Unguja, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, akimsikiliza Mkurugenzi wa (BOT) Tawi la Zanzibar Camillus Kombe,wakati akitembelea banda la maonesho la (BOT) katika viwanja vya Maonesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi “B”, wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi na (kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla,wakimsikiliza Katibu Msaidizi wa Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC) Jonas Nduttu, wakati akitembelea banda la maoneshe la (JFC) wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
WASANII wa Kikundi cha Ngoma ya Kiumbizi  kutoka Pembe Kijiji cha Pujini wakitowa burudani ya wakati wa Uzinduzi wa Maadhimishio ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliofanyika katika viwanja vya Moanesho Nyamanzi Dimani Ndambani Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo 14-4-2024.

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye nyanja zote za maendeleo, kisiasa, Uchumi, utamaduni na huduma za jamii yameipatia nchi heshima kubwa kwenye Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi wakati wa uzinduzi wa Sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema, kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano huo, Tanzania imeendelea kubaki kwenye historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote kutokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano viliyoasisiwa na viongozi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano huo.

“Tunaposherekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tuna wajibu wa kujipongeza kwa mafanikio makubwa nchi yetu iliyoyafikia kwenye nyanja zote za maendeleo kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii. Alisifu Dk. Mwinyi.

Alieleza dhamira ya dhati kwa viongozi mbalimbali walioshika nyadhifa za uongozi kwa awamu tofauti kwa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza maono ya Waasisi wa Taifa hili kumefanikisha kudumisha na kuimarisha Muungano huo.

“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo umeongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu” Alisifu Rais Dk. Mwinyi.

Akizungumzia changamoto za Muungano, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote za Muungano huo, ikiwemo kuunda Tume na Kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja za Muungano.

Alisema, miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.

Alisema tangu mwaka huo hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa, kati ya hoja hizo alieleza hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Aidha, hoja zilizobaki Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa zipo kwenye hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
 
Dk. Mwinyi pia alieleza Imani yake na kwa utashi wa dhamira ya dhati ya Serikali za pande zote mbili kwamba hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.

“Ni wajibu wetu sote kuulinda, kuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi ili tuzidi kunufaika sisi tuliopo leo pamoja na vizazi vyetu kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu” Alisihi Rais Dk. Mwinyi.

Alieleza ndani ya kipindi miaka mitatu (2021 -2024) hoja 15 pia zilipatiwa ufumbuzi, kati ya hoja 18 zilizokuwepo.

Alisema, utatuzi wa changamoto za Muungano, umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zote mbili za SMZ na SMT kwa kuimarisha na kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu uliopo ambao ni Tunu muhimu na fahari ya Tanzania

Hata, hivyo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuimarisha Muungano na kuwa ni moja ya vipaumbele vyake.

Sambamba na kuwahakikishia Watanzania wote kwamba Serikali za SMZ na SMT zitaendelea kuchukua hatua ili taifa la Tanzania liendelee kusonga mbele kwa maendeleo na kuendelea kubaki kuwa nchi ya amani na utulivu.

Rais Dk. Mwinyi pia alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wenziwe na Wananchi wote wa Tanzania kuendelea kuulinda Muungano huo ili waendelee kuishi kwa amani na kuzidi kujiletea maendeleo binafsi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla aliwashukuru Rais Dk. Mwinyi na Dk. Samia kwa namna wanavyoliongoza taifa kwa misingi ya kusimamia Muungano.

Aidha, umuhimu wa kuendelea kulindwa Muungano kuenziwa, kuimarishwa na kulindwa kwa maslahi ya Watanzania.

Alieleza, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ofisi ya Muungano na Mazingira ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanawajibu wa kuielewaja jamii juu ya historia ya Muungano kwa vizazi viliopo sambamba na kuwasihi Watanzania kuendelea kuu Watanzania.

Mapema akizungmza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk. Selemani Saidi Jafo alisema historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeundwa na sababu nyingi hadi kufikia kusainiwa kwa hati ya Muungano mwaka 1964 chini ya waasisi wake Hayati baba wa Taifa Julius K. Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Akitaja baadhi ya sababu hizo zikiwemo urafiki na udugu wa damu wa Wananchi wa pande mbili za Muungano, lugha ya Kiswahili iliyowaunganisha watu wa pande mbili hizo, pamoja vyama vya ukombozi vya TANU na ASSP Waziri Jafo alieleza kwamba vilitoa mchango mkubwa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Alisema katika kusheherekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wanatarajia kuzindua kitabu maalum kinachoeleza historia ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya kufundishiwa Skuli za Sekondari nchi nzima.

Uzinduzi wa sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na Ufunguzi wa Maonesho maalum ya Taasisi za Muungano chini ya kaulimbiu, “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, unaashiria kuanza rasmi kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti, usafi wa mazingira na ushiriki wa wananchi na viongozi kwenye matukio ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi kwa maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Pia uzinduzi huo unaashiria hatua za maendeleo kwenye upatikanaji wa fursa kwa Taasisi za Muungano na zisizo za Muungano, Makampuni na wajasiriamali ili kuionesha jamii huduma na bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika shughuli zao.

Kilele cha sherehe hizo ni tarehe 26 Aprili, 2024 kwenye viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Posted by MROKI On Sunday, April 14, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo