Mkurugenzi wa Ununuzi Wizara ya Nishati, Bi. Marieta Kiago ametoa rai kwa Wanawake hususan vijana kuwa wanapopata nafasi za kufanyakazi kwenye maeneo na Taasisi mbalimbali kuhakikisha wanasimama imara na kuitenda haki kwa wananchi.
Bi. Kiaho ameyasema hayo alipokuwa akielezea nafasi ya Msichana katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo nchini yatafanyika mkoani Arusha.
"Ninachotaka kusema katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani wale tunaopata nafasi basi tuzitendee haki hasa tunapotoa huduma kwa wananchi." Amesema Bi. Kiago
Amesema miaka ya nyuma hakukuwa na haki kwa wanawake katika masuala mbalimbali tofauti na sasa ambapo haki za mwanamke zinazidi kutambuliwa na kuheshimiwa.
Akizungumzia kuhusu usawa Bi. Kiago amesema unatakiwa kuwepo katika jinsia zote kwa wanawake na wanaume ambapo ameipongeza Serikali kwa kuweka usawa katika utekelezaji wa majukumu kwenye jamii.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanawake wengi wameshika nafasi mbalimbali za uongozi akitolea mfano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
0 comments:
Post a Comment