Nafasi Ya Matangazo

January 31, 2025


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga akizungumza na uongozi wa Gereza la Wilaya ya Babati mara baada ya kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa utumiaji wa Nishati safi ya kupikia gerezani hapo.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Solomoni Mwambingu na Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Manyara akitoa taarifa kwa Mhe. Sendiga mara baada ya kumaliza kufanya ukaguzi.

Na Cathbert Kajuna- Kajunason Blog/Michuzi TV

Manyara Januari 30, 2025: Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendigaametembelea Gereza la Wilaya ya Babati na kukagua utekelezaji wa utumiaji wa nishati safi ya kupikia gerezani hapo. 

Akitoa taarifa kwa Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi wa jeshi la Magereza Solomoni Mwambingu na Mkuu wa jeshi la Magereza Mkoa wa Manyara amesema hadi kufikia mwaka jana Disemba 2024 waliweza kutekeleza maagizo ya Serikali kwa asilimia mia moja (100%) na Magereza yote katika Mkoa wa Manyara yanatumia Nishati safi ya kupikia.
Baada ya kupokea taarifa hiyo na kufanya ukaguzi na kuona namna mitambo ya nishati safi inavyofanya kazi katika gereza hilo RC Sendiga, amewapongeza Jeshi la Magereza Manyara kwa utekelezaji huo wa maagizo ya Serikali kikamilifu.

Aidha, RC Sendiga ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwasisitiza wananchi na taasisi za umma na binafsi katika Mkoa kutumia nishati safi ili kulinda afya zao dhidi ya hewa na moshi unaotokana na matumizi ya Nishati zisizo safi na salama kwa binadamu ikiwemi kuni na mkaa.
Posted by MROKI On Friday, January 31, 2025 No comments


Na Mariam Hassan, Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, ameitaka Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kuhakikisha watumishi wote wa makao makuu ya Halmashauri hiyo wawe wamehamia kwenye jengo jipya la ghorofa moja ifikapo tarehe 15 Machi 2025.

Wakili Mtatiro ametoa maelekezo hayo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika Halmashauri hiyo, kupokea mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Wakili Mtatiro amesisituza kuwa ikifika 15 Machi, ataongoza yeye mwenyewe kazi ya uhamaji kwani kwa miaka kadhaa sasa Halmashauri imekuwa ikisuasua kuhama.

Wakili Mtatiro amezungumza kwa simu na kutoa ufafanuzi zaidi kuwa tangu mwaka jana Halmashauri iliahidi ingehamia katika jengo jipya na kwamba vifaa vyote vya upauaji kama madirisha vilikuwa vimeshakamilika lakini hadi leo kumekuwa na kusuasua.

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga linatarajia kupitisha Mpango wake wa Bajeti wiki ijayo.
Posted by MROKI On Friday, January 31, 2025 No comments








Na: Mwandishi Wetu, Tanga


Wananchi wa Tanga wamebariki kwa asilimia 100 azimio la Mkutano Mkuu wa CCM Taifa lililompitisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya Urais kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Hayo yameelezwa na  Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM) Ummy Mwalimu kwa niaba ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Januari 28, 2025 katika viwanja vya Community Centre jijini Tanga. 

Ummy amesema maamuzi ya Mkutano Mkuu ni sahihi kutokana na kazi nzuri na kubwa zilizofanywa na Rais Dk. Samia na Dk. Hussein Mwinyi huku wakitekeleza ipasavyo ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 katika kutatua kero za wananchi na kukuza maendeleo nchini.

"Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, ndugu zangu wa Tanga, naweza kusema ninayo mamlaka ya kusema kwamba, sisi wananchi wa Tanga Mjini ambao ndiyo wapigakura tunapongeza na kuunga mkono maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa wa kumpitisha Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka 2025. 

Pia tunaunga mkono maamuzi ya kumpitisha Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea Urais Kwa upande wa Zanzibar na ndugu yetu, shemeji yetu Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu," amesisitiza Ummy Mwalimu.

Sanjari na hilo, Ummy Mwalimu amesema kazi zilizofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan zinaonekana kwa macho na ndiyo maana katika mkutano huo makundi yote ya watu kama vile bodaboda, wavuvi, wajane, vijana, madereva wa magari wamehudhuria mkutano huo.

Katika hatua nyingine, Ummy Mwalimu amesema CCM ina mtaji wa kura za wananchi kwa sababu katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, CCM ilipata ushindi wa asilimia 100 ambapo mitaa yote 181 ya Tanga Mjini inaongozwa na wenyeviti wa mitaa watokanao na CCM. 

Aidha, kazi nzuri zilizofanyika Tanga Mjini hasa katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, umeme, utoaji mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum, ni dhahiri CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu.

Mkutano huo pia umetumika kuzindua rasmi maandalizi ya maadhimisho ya miaka 48 tangu kuzaliwa CCM ambapo viongozi mbalimbali wa chama na serikali ngazi ya mkoa na wilaya wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ustadhi Rajab Abdurahmani, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dk. Batilda Buriani na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Hamisi Mkoba na wengine walipata fursa ya kuhutubia huku msisitizo mkubwa ukiwa ni kazi nzuri zilizofanywa na CCM katika kuwahudumia wananchi wake na kusukuma agenda ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi.
Posted by MROKI On Friday, January 31, 2025 No comments

Na Cathbert Kajuna - Kajunason Blog/Michuzi TV, Manyara.

Mkuu wa mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga (kwanza kushoto) leo Januari 29, 2025 amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Bw. Michael John Semindu aliyeteuliwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Ofisi ya  mjini Babati, Manyara.

Hafla hiyo ya uapisho ilihudhuriwa na Wakuu wote wa Wilaya (5) za Mkoa wa Manyara, wakuu wa vyombo vya ulinzi na Usalama.

Akizungumza na Wakuu wa Wilaya mara baada ya uapisho Mkuu Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga alitoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya mpya na kumshukuru  Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi alioufanya.
Mhe. Sendiga aliweza kuwaelekeza Wakuu wa Wilaya hao vipaumbele vyake katika utendaji wa kazi ikiwemo ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia Wananchi wake na kuleta maendeleo katika Taifa, usikilizaji na utatuzi wa kero za Wananchi kuanzia Ngazi ya Mtaa mpaka katika Halmashauri zao, kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti Uhalifu, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Sambamba na hayo amesema; “Nendeni mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze matarajio ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo.”
Aidha Mhe. Sendiga amewaagiza wakuu wa wilaya Mkoani humo kushirikiana na jamii katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na wanaume kwani kumekuwepo na malalamiko juu ya wanaume kupigwa na wake zao hasa wilayani Hanang'.
Mhe. Sendiga amesema wakuu wa wilaya wanawajibu wa kuelimisha jamii juu ya ukatili wa kijinsia bila kuwasahau wanaume ambao nao wamekuwa wahanga wakubwa wa vipigo kutoka Kwa wake zao.

Naye mkuu wa wilaya ya Hanang' Mhe. Almishi Azal amekiri kuwepo kwa matukio ya wanaume wengi kunyanyaswa na wake zao.

Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael John Semindu aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyoagizwa na mkuu wa Mkoa na kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga (wa tatu kutoka kulia) akifurahi pamoja na Wakuu wa Wilaya, kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhe. Fakii Raphael Lulandala, Mkuu wa Wilaya ya Hanang' Mhe Almishi Issa Hazal, Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Emmanuela Kaganda. Wa kwanza kutoka kushoto ni  Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema pamoja na Mkuu Mpya wa Wilaya ya Mbulu Mhe. Michael John Semindu.
Wanahabari wakiwa katika picha na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbert Sendiga (wa tatu kutoka kushoto waliokaa pamoja na baadhi ya viongozi wa mkoa.
Posted by MROKI On Friday, January 31, 2025 No comments

January 30, 2025

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) akichangia kwenye kikao maalum cha Mawaziri mbalimbali duniani (Ministerial Roundtable) katika Mkutano wa Kimataifa  kuhusu Soko la ajira tarehe 29 Januari, 2025 Jijini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Akizungumzia wakati akichangia hoja iliyowasilishwa kuhusu maendeleo ya vijana na mabadiliko sasa, Mh. Kikwete alishukuru Ushirikiano uliopo baina ya wadau wa maendeleo ya kazi bila kusahau miongozo na mabadiliko ambayo yamefanyika nchini Tanzania ikiwemo mikakati ya kukuza ujuzi, matumizi ya Tehama, mkazo katika miradi inayotoa ajira nyingi na ile ya kimkakati. 

Mkutano huo unawakutanisha Mawaziri wa Kazi na Ajira kutoka nchi zaidi ya 45 duniani kujadili na kuweka mikakati ya kuongeza kazi za staha kwa Vijana kwa kuzingatia mchango wa sayansi na teknolojia.




Posted by MROKI On Thursday, January 30, 2025 No comments




Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Leo Januari 30, 2025 mkoani Geita, maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga miili ya wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe waliofariki kwa kupigwa na radi mnamo tarehe 27 januari, 2025.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameongoza shughuli za kuaga na kukabidhi ubani kwa wafiwa huku akiwataka kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki cha majonzi.

Ametoa pole kwa wazazi, walezi ndugu wa watoto pamoja na wanafunzi wa Businda kwa kuondokewa na wapendwa wao na wanajamii wa Businda Sekondari kwa jitihada na utoaji wa huduma wakati wa tukio hilo.

“ Imeandikwa kwamba shukuruni Mungu kwa kila jambo, Mungu ametukutanisha leo katika hali ya majonzi. Tukio hili litukumbushe kutenda mema wakati wote na tuamini kwamba Mungu ndiye mwenye uweza. Kipekee ningetamani kuwataja Madaktari wote kwa majina kutokana na msaada mkubwa walioutoa lakini itoshe kusema asante
kwa kazi kubwa mliyoifanya” amesema Dkt. Biteko.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito amekuwa akifuatilia kwa karibu na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuzifariji familia za wafiwa, wana Bukombe na Taifa kufuatia kuondokewa na vijana waliokuwa katika safari ya kutafuta elimu.

“Rais Samia amegharamia msiba pamoja na kutoa ubani kwa kila familia za wafiwa pamoja na kugharamia usafirishaji wa miili ya wanafunzi wawili kwenda Chato, Geita na Karatu mkoani Arusha kwa mazishi.

Viongozi mbalimbali wa dini wamewapa faraja wafiwa na kusema msiba haujawahi kuzoeleka lakini kwa mapenzi ya Mungu atakuwa mfariji wao.

Viongozi hao wamewataka wanadamu kujipanga wakati wote kwa kuwa hawajui ni wakati gani utafikwa na umauti kutokana na fumbo aliloliweka Mwenyezi Mungu.

Aidha, wamemwomba Mungu awape uvumilivu viongozi katika kipindi hiki cha majonzi.

Wanafunzi hao saba waliokuwa wakisoma kidato cha tatu walikuwa na umri kati ya miaka 16 na 18, walikutwa na umauti kwa kupigwa na radi wakati wakiendelea na masomo darasani.

Waliofariki ni Erick Emmanuel Akonaay (17), Nikas Paul Tompoli (18) Gabriel Daud Makoye (17), Doto Marco Masasi (18), Asteria Reonard Mkina (16), Peter Nkinga Manyanda (17) na Erick Martine Bugalama (16)

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Theodora James Mushi amesema  wanafunzi hao walipatwa na umauti wakiwa katika harakati za kusaka elimu.

Wanafunzi wanne kati yao walifariki papo hapo na wengine watatu walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali na vituo mbalimbali vya Afya.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskazi Mragili ameishukuru Idara ya afya kwa utayari na uharaka wa utoaji huduma kwa wanafunzi wote 138 ambapo wanafunzi 89 waliathirika moja kwa moja na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani. Majeruhi wote wameruhusiwa na wale waliopata majeraha wanaendelea kutibiwa wakitokea nyumbani.
Posted by MROKI On Thursday, January 30, 2025 No comments


 

Posted by MROKI On Thursday, January 30, 2025 No comments
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko  amesema uunganishaji wa umeme kwenye maeneo ya Vijiji ni shilingi 27,000/- na maeneo ya Vijiji mji ni shilingi 320.960/-.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Januari 30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Bukene, Mhe. Selemani Zedi aliyetaka kufahamu kwa nini maeneo ya Bukene na Itobo hayaunganishiwi umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000/-.

"Mheshimiwa Spika maeneo ya Bukene na Itobo ni Vijiji Mji ambapo gharama ya kuunganisha umeme maeneo ya Vijiji Mji ni shilingi 360.960," Amesisitiza Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuangalia kama kuna uwezekano wa kufanya maboresho kulingana na tathmini amabayo imefanyika. 

Aidha, Mhe. Kapinga amesema tayari amemuagiza Meneja wa Mkoa wa Tabora na wa Wilaya ya Nzega kufanya tathmini ya kina ili yaweze kupatikana majibu ya kina iwapo maeneo ya Bukene na Itobo ili kuweza kuondoa mkanganyiko uliopo.

Akijibu swali Mbunge wa Kilombero, Mhe. Abubakari Asenga aliyetaka kufahamu kwa nini maeneo ya Katinduka bado yanalipia umeme kwa shilingi 360.960/- wakati ni maeneo ya Vijiji, Mhe. Kapinga amesema. maeneo ya Vijiji yanaunganishwa kwa shilingi 27,000/- kutokana na Serikali na wafadhili kutoa fedha za kutekeleza miradi ya umeme Vijijini.

Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa sio kila eneo linakidhi vigezo vya kuunganisha umeme kwa shilingi 27,000/- nae neo Katinduka ni maeneo ya Mtaa.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest, aliyetaka kufahamu ni lini Vijiji vilivyobaki Kyerwa vitafikiwa na huduma ya umeme kikiwepo Vijiji vya Buganza na Nyarigongo, Mhe. Kapinga amesema maeneo ya Kyerwa umeme umeshafika katika makao Makuu ya Vijiji na kuongeza kuwa Mkandarasi anaendelea na kazi katika kilometa mbili za ziada.
Posted by MROKI On Thursday, January 30, 2025 No comments

January 29, 2025

Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe leo Jumanne Januari 28, 2025 amezindua mitambo maalum na malori mawili mapya, yaliyonunuliwa na Halmashauri hiyo kwaajili ya ukarabati wa barabara za mitaa ya Jiji hilo, akitoa wito wa matunzo ya mitambo hiyo ili iweze kudumu na kutumika kwa muda mrefu.

Wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Iranqhe mbele ya Wananchi wa Jiji la Arusha ameelekeza pia Kila Kata kukabidhiwa shilingi Milioni 4, kwaajili ya manunuzi ya vifusi vya kujengea barabara hizo, ikiwa ni fedha baki kwenye bajeti ya Shilingi Bilioni 2 zilizokuwa zimetengwa awali kwenye manunuzi ya Mitambo ya ujenzi wa barabara hizo.

Katika hatua nyingine, Mstahiki meya pia amehimiza suala la utunzaji wa mazingira, akiwasihi madiwani kusimamia ajenda hiyo ya upandaji wa miti kwa wingi hasa katika maeneo yanayokumbwa na ukame huku pia akitahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la utupaji wa taka mitaani hasa chupa za Plastiki zinazozagaa kwenye mitaro na maeneo mbalimbali ya wazi suala linalodumaza sifa ya Mkoa wa Arusha kuwa Kitovu cha Utalii kwa Tanzania bara.

Awali katika maelezo yake, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Ndugu John Kayombo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Mhe. Iranqhe, amesema mitambo hiyo itakwenda kujenga na kukarabati barabara za mitaa yote 154, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa kuhakikisha Arusha inanufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.











 

Posted by MROKI On Wednesday, January 29, 2025 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo