Nafasi Ya Matangazo

August 01, 2021

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akiangali moja ya kazi zinazofanywa na Vyuo vikuu nchini  alipotembelea mabanda ya maonesho wakati wa kufunga maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam
Mmoja wa washiriki wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia akipokea cheti cha utambuzi wa kushiriki maonesho hayo kwa mwaka 2021.
Waombaji wa vyuo vya Elimu ya Juu wakifanyiwa udahili wa moja kwa moja kutoka kwenye mabanda ya maonesho ya   Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (hayupo pichani) wakati wa kufunga maonesho hayo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
**********
NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga (Mb) amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Sekta ya Elimu ya Juu imepata mafaniko makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la udahili na uimarishaji mifumo ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.

Naibu Waziri Kipanga amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema idadi ya wanafunzi wa Shahada ya kwanza kwenye vyuo vya Elimu ya juu imeongezeka kutoka 65,064 mwaka 2015/16 hadi 87,934 mwaka 2020/21 huku wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wakiongezeka kutoka wanafunzi 125,126 mwaka 2015 hadi 132,392 mwaka 2020.

Ameongeza kuwa katika  kuhakikisha Vyuo Vikuu vinatoa elimu bora ya kiushindani ndani na nje ya Nchi, mifumo ya uthibiti ubora imeendelea kuimarishwa ikiwemo  mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji na mifumo ya uhakiki na utambuzi wa sifa za kitaaluma za wahitimu wa Elimu ya Juu zilizotolewa na vyuo vya nje ya nchi. 

“Pamoja na mafaniko hayo makubwa pia tumeboresha  miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, kumbi za mihadhara, maabara, maktaba, hosteli na ununuzi wa vifaa vya utafiti, pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia,” amesema Mhe. Kipanga.

Aidha Naibu Waziri Kipanga ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu kuendelea kufanya mapitio ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira kwa kuweka msisitizo katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), pamoja na utoaji wa mafunzo kwa vitendo. 

Pia amendelea kuvitaka  vyuo hivyo kuweka mikakati ya kuzalisha wataalamu wa kutosha hususani katika sekta adimu na zenye tija kwa maendeleo ya nchi yetu ili kufikia lengo la kitaifa la kuwa na wahitimu 98,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025/26.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa amesema maonesho ya mwaka 2021 yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kupata washiriki wengi na kwamba zaidi ya waombaji elfu 52 wa Shahada ya kwanza  wametuma maombi katika vyuo mbalimbali na kati ya maombi hayo mengine yamefanyika moja kwa moja kupitia maonesho. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi waliohitimu kidato cha sita ambao wangependa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, wameipongeza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania kwa kufanya maonesho hayo kwa kuwa wamepata fursa ya kukutana na vyuo vyote katika eneo mmoja na kufanyiwa udahili bila gharama yoyote.
Maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoanza *Julai 26* na kuhitimishwa Julai 31 yalikuwa na kauli mbiu isemayo “Kuendelea Kukuza na Kudumisha Uchumi wa Kati kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia”.
Posted by MROKI On Sunday, August 01, 2021 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo