Nafasi Ya Matangazo

July 01, 2019

Meza kuu watatu kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambaye ni mgeni wa heshima na Mkuu wa Nchi pekee kutoka Bara la Afrika akiwa katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika. Wa pili kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje China na Mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi. Mkutano huo umefanyika Beijing,China na Kuhudhuriwa na Mawaziri wa mambo ya Nje wa Nchi za Afrika 53. Juni 25, 2019.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi (Mb) (katikati) akifuatilia mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC),Beijing - China. Juni 25,2019 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.) (watano kutoka kushoto) akiwa katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaohudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje 53 kutoka Nchi za Afrika. Mkutano huo unafanyika Beijing – China. Juni 25, 2019.
Sehemu ya Mawaziri wa mambo ya Nje kutoka Nchi 53 za Afrika wanaohudhuria mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).Mkutano huo unafanyika Beijing – China. Juni 25, 2019.
BOFYA HAPA KUONA ZAIDI.

*****************
Nchi za Kiafrika zimeiomba China kuhakikisha kuwa ufadhili ama mikopo inayotoa kwa Nchi za Kiafrika inalenga katika miradi ya kikanda itakayoziunganisha na kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi huku Tanzania ikiitaka China kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inayowekeza nchini iwe ya manufaa kwa pande zote mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameyasema hayo Beijing Nchini China katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) alipopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo na kuongeza kuwa endapo China itazisaidia kwa ufadhili ama kwa mikopo nafuu kuwekeza katika miradi hasa ya miundombinu itakayoziunganisha Nchi za kiafrika kwa kiasi kikubwa itazisaidia Nchi hizo kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe  itaziwezesha kupiga hatua za kimaendeleo na kiuchumi na hivyo kujitegemea.

Ameongeza kuwa Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umekuwa ni wa manufaa kwa kuwa Nchi zenyewe za kiafrika zimepata fursa ya kutaja baadhi ya miradi ya kipaumbele kutokana na uhitaji wa Nchi husika  huku akiitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji kwa kuwa Nchi nyingi za Kiafrika bado zina vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kuzalisha umeme ambao utakuwa ni wa bei nafuu na kusaidia katika ujenzi wa viwanda.

Aidha, katika mkutano huo wa siku mbili uliozikutanisha Nchi zipatazo 53 za Kiafrika na China zimeitaka China pia kuhakikisha inasaidia ama kufadhili katika kuinua uwezo wa kitaaluma utakaowawezesha vijana kwa Kiafrika kujiajiri na kupata wataalam wabobezi katika masuala mbalimbali kutokana na uwekezaji hasa wa viwanda na miundombinu utakaofanywa kwa pamoja na China na Nchi za Kiafrika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amesema katika mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Tanzania imesisitiza kuwa katika miradi ya uwekezaji ya misaada ama ile ya mikopo nafuu inayoelekezwa Tanzania iwe ni ile yenye manufaa kwa pande zote mbili yaani win-win situation kama anavyosisitiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa China Mhe. Xi Jimping, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi amesema kuwa China haitatoa misaada yenye masharti magumu kwa Nchi za Afrika, badala yake itaendeleza ushirikiano wake na Afrika katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo, Serikali ya China imeahidi kuongeza umoja na ushirikiano kati yake na Afrika katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na usalama  ili kuleta maendeleo endelevu kwa watu na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.

Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika limeazimia kwa pamoja kutekeleza miradi ya kipaumbele kulingana na uhitaji wa kila nchi kwa kufuata hatua nane zilizotangazwa katika mkutano wa wakuu wa nchi wa FOCAC uliofanyika mwezi September 2018 jijini Beijing.

Hatua hizo ni pamoja na program ya kuendeleza viwanda kupitia ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda, ujenzi wa miundombinu ikiwemo nishati, reli, barabara na bandari, sambamba na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vitakavyosaidia kuzalisha nguvu kazi ya viwandani.
Posted by MROKI On Monday, July 01, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo