Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na  viongozi wengine meza kuu  wakishuhudia makabidhiano ya Mfumo wa Kudhibiti Mawasiliano ya Ndani na Nje ya Nchi (TTMS) baina ya wakandarasi Bw. James Gabriel Claude CEO wa kampuni ya GVG na Samuel Kiki Gyan Mkurugenzi wa kampuni ya SGS na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA  Dkt. James Kilaba katika hafla iliyofanyika makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dar es salaam leo Januari 18, 2019.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 18 Januari, 2019 ametembelea miundombinu ya mfumo wa kuratibu na kusimamia mawasiliano yote ya simu (Tele-Traffic Management System – TTMS) na kushuhudia makabidhiano ya mfumo huo kutoka kampuni za ukandarasi za Societe Generale de Surveillance S.A (SGS)na Global Voice Group S.A (GVG), na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika Makao Makuu ya TCRA Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, viongozi wa siasa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

Mfumo huo umewekwa kwa malengo ya kupata takwimu za mawasiliano ya simu yanayofanyika ndani na nje ya nchi, kuhakiki mapato yote ya watoa huduma za mawasiliano nchini, kupata takwimu zinazohusiana na matumizi ya huduma za mawasiliano (simu za sauti, data na ujumbe mfupi), kugundua mawasiliano ya simu za ulaghai na kutambua takwimu za ada za miamala ya fedha mtandaoni. 

Malengo mengine ni kusimamia ufanisi wa ubora wa huduma, kutambua taarifa za laini za simu, kubaini na kufungia simu zenye namba tambulishi zilizonakiliwa na kuwasilisha kwa Serikali mapato yanayotokana na mawasiliano ya simu za kimataifa zinazoingia na kuishia hapa nchini. 

Akizungumza baada ya kushuhudia makabidhiano hayo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TCRA kwa kupata miundombinu hiyo na ameitaka mamlaka hiyo kuhakikisha inajijengea uwezo wa kuusimamia, kuuendesha, kuuboresha, kupanua uwigo wake na kuulinda ili uweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa. 

Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa mara alipoingia madarakani baada ya kubaini kuwa mkandarasi alikuwa ameweka mfumo ambao ulitoa mwanya wa kushindwa kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya Serikali na amebainisha kuwa sasa ana uhakika nchi itanufaika ipasavyo kwa kukusanya mapato yote yanayostahili kutokana na mawasiliano. 

“Tangu mfumo huu uanze tumeweza kufahamu idadi ya watumiaji wa simu na data nchini kwa urahisi, tumepunguza kiwango cha udanganyifu kwenye simu za kimataifa kutoka asilimia 65 hadi 10 na hivyo kutuwezesha kupata chanzo kipya cha mapato, Serikali imepata shilingi Bilioni 93.665, hiki ni chanzo kipya kabisa, ambacho zamani hakikuwepo” amesema Mhe. Rais Magufuli. 

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba kwa kazi nzuri aliyoifanya kusimamia uwekaji wa mfumo huo na amemtaka yeye na wafanyakazi wote wa TCRA kuendelea kuchapa kazi bila woga ikiwemo kusimamia upatikanaji wa mapato ya Serikali na kudhibiti wahalifu wa kimtandao watakaobainika kupitia mfumo huo. 

Mhe. Rais Magufuli amesema amepata taarifa kuwa kati ya taasisi 667 za Serikali zinazostahili kuunganishwa na mfumo mkuu wa ukusanyaji wa fedha za umma (Government e-Payment Gateway – GePG) ni taasisi 339 tu ndizo zimeunganishwa na hivyo ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha taasisi hizo zinaunganishwa haraka ili kuongeza ukusanyaji wa mapato, kuondoa urasimu, kupunguza gharama kubwa za ufuatiliaji na kuepusha vitendo vya rushwa. 

Mapema katika maelezo yake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba amesema mfumo wa TTMS ulianza kufungwa mwaka 2013 na tangu wakati huo wakandarasi wamefanya kazi kwa ushirikiano na wafanyakazi wa TCRA ambao sasa wanaouwezo wa kuundesha na pia kihifadhi taarifa (Saver) kipo hapahapa nchini. 

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema mfumo wa TTMS umekuwa nyenzo muhimu ya kiukaguzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kampuni za simu, na kwamba katika kipindi cha kipindi cha Januari hadi Desemba 2018ilibainika kuwa miamala ya fedha kupitia simu za mikononi ilifikia shilingi Trilioni 139.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35.2 ikilinganishwa na mwaka 2017. 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe amesema uwekaji wa mfumo TTMS ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015, na kwamba pamoja na kuweka mfumo wa kuongeza mapato pia Serikali imeendelea kupunguza gharama za mawasiliano ambapo gharama za kupiga simu kwa dakika zimepungua kutoka shilingi 30.8 hadi shilingi 10.4 na ifikapo 2022 zitafikia shilingi 2. 

Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuweka msukumo mkubwa katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kupitia simu za mkononi na kwamba mafanikio ya kuweka mfumo huo yaliyotokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Bunge, yamedhihirisha kuwepo ushirikiano mzuri wa Serikali na Bunge na uimara wa Bunge.
Posted by MROKI On Friday, January 18, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo