Nafasi Ya Matangazo

August 10, 2018


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt aliyemtembelea akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuonesha albamu ya picha Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza (Department of International Development - DFID - ) Mhe. Penny Mordaunt inayoonesha Shule ya Sekondari ya Ihungo iliyobomolewa kabisa na tetemeko la ardhi Setemba 10, 2018  ambayo imejengwa upya na serikali ya Uingereza kupitia mpango wake wa maendelo ya elimu kupitia UKAid/DFID. Picha hizo zinaonesha shule hiyo baada ya tetemeko, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi siku ya mwaka mpya wa 2017 na inavyoonekana sasa baada ya kujengwa upya. Mhe. Mordaunt, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi, alimtembelea  Rais Dkt. Magufuli akiwa ameongozana na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. Sarah Cooke, na Mkuu wa ofisi ya DIFD nchini Mama Beth Arthy Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 10, 2018
Uingereza imetoa msaada wa shilingi Bilioni 307.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika elimu, mapambano dhidi ya rushwa na uboreshaji huduma za afya.

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza Mhe. Penny Mordaunt ametangaza msaada huo leo tarehe 10 Agosti, 2018 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Penny Mordaunt amesema fedha hizo zinatolewa kwa ajili ya kuunga mkono vipaumbele vya Mhe. Rais Magufuli ambapo kati yake shilingi Bilioni 124.5 zitaelekezwa katika kuinua ubora wa elimu hususani kutoa fursa ya elimu kwa watoto wa kike na wenye ulemavu, shilingi Bilioni 23.5 zitaelekezwa katika kuunga mkono juhudi za kupambana na rushwa, na shilingi Bilioni 160 zitaelekezwa katika kuboresha huduma za afya.

“Tunafanya hivi ili kudhihirisha dhamira yetu ya kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wetu, tunataka kujielekeza katika kuhakikisha Mhe. Rais Magufuli anafanikisha ahadi zake kwa Watanzania na tunafurahi kuwa wadau muhimu wa hilo” amesema Mhe. Penny Mordaunt.

Ameongeza kuwa pamoja na kuwa wachangiaji wakubwa katika bajeti ya Serikali, Uingereza ni nchi inayoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na kwamba wanafurahishwa na wito wa Mhe. Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara zaidi kutoka Uingereza watakaowekeza kwa manufaa ya pande zote (win-win).

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Penny Mordaunt kwa msaada huo na amemuomba kufikisha shukrani zake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa mchango mkubwa ambao Uingereza hutoa kuchangia bajeti ya Serikali na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Namshukuru sana Waziri Penny Mordaunt kwa kutambua juhudi zetu za kuinua elimu, kupambana na rushwa na ufisadi pamoja na kuboresha huduma za afya, msaada huu utatusaidia kuongeza nguvu kwa sababu watoto wakipata elimu bora, tukikomesha rushwa na watu wetu wakiwa na afya njema tutaweza kujenga viwanda na kukuza uchumi wetu kwa kasi zaidi” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amemuahidi Mhe. Penny Mordaunt kuwa fedha zilizotolewa kiasi cha shilingi Bilioni 307.5 zitatumika vizuri na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha uhusiano wa Tanzania na Uingereza unazidi kuimarishwa kwa kuwa inatambua kuwa Uingereza ndio mwekezaji mkubwa hapa nchini na imekuwa ikitoa misaada mikubwa ya fedha za walipa kodi wa Uingereza kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

Pia, Mhe. Rais Magufuli amemkabidhi Mhe. Penny Mordaunt albamu ya picha za shule ya sekondari Ihungo mkoani Kagera iliyojengwa upya baada ya kuharibika vibaya kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 2016, na ameishukuru Uingereza kwa msaada wa shilingi Bilioni 6zilizotumika kujenga majengo hayo kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini Mhe. Sarah Cooke na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambaye amesema ziara ya Waziri Penny Mordaunt imezidi kukuza uhusiano wa Tanzania na Uingereza.

Posted by MROKI On Friday, August 10, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo