Nafasi Ya Matangazo

January 19, 2018

Mwandishi Wetu, TJNCDF

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Tanzania (TANCDA) limetoa maelekezo muhimu kwa jamii katika kufanikisha suala zima la kuepuka au kudhibiti magonjwa sugu.

Magonjwa sugu yanayoelezewa na TANCDA ni yale yasiyo ya kuambukiza na ikajikita kwenye magonjwa manne makuu ambayo yamekuwa yanawasumbua wengi, hasa katika nchi masikini.

Magonjwa hayo sugu ni: Moyo na mishipa ya damu, njia ya hewa na mapafu, kisukari na saratani.

Makamu Mwenyekiti wa TANCDA, Profesa Andrew Swai anasema kuwa kutibu magonjwa haya kunatumia fedha nyingi hivyo anaishauri jamii kuchukua tahadhari ya kuepukana nayo.

Kwa wale ambao tayari wameambukizwa, Profesa Swai anasema wanapaswa kufuata kikamilifu maelekezo ya madaktari hospitalini ili kuyadhibiti kikamilifu.

Zipo njia nyingi za kukabiliana na magonjwa haya lakini kwa hapa TANCDA inatoa elimu juu ya mtindo bora wa maisha kwa kupangilia vizuro mipango ya mlo na kuhakikisha chakula unachotumia ni cha kuboresha afya. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.

TANCDA inaeleza kuboresha mpango wako wa kula huimarisha afya na kuuweka mwili katika hali ya kuimarika dhidi ya magonjwa sugu.

Kwa sababu hiyo, TANCDA inataja mambo 12 ya kuzingatia kukabili kisukari, saratani, njia ya hewa na mapafu pamoja na matatizo ya mishipa na moyo.

Moja, Unapaswa kula mlo kidogo, mara kwa mara badala ya mlo mmoja au miwili mikubwa. Jambo jingine la kuzingatia ni kutopitisha muda wa kula.

Pili, Kuwa na mazoea ya kunywa maji badala ya chai au vinywaji vyenye sukari. Inakadiriwa kuwa chupa moja ya soda ina vijiko tisa au zaidi vya sukari. 

Tatu, epuka kula mafuta ya wanyama. Inapendekezwa kutumia mafuta ya mimea kwa ajili ya kupikia.

Nne, mafuta ya kupikia yasizidi kijiko kimoja cha chai kwa siku na kumbuka kuna mafuta kwenye aina nyingi za vyakula kama vile keki, biskuti, soseji na baga. 

Tano, choma, oka au chemsha chakula, epuka vyakula vya kukaanga kama vile chipsi, sambusa na mandazi.

Sita, Samaki, nyama ya ndege wa kufugwa na aina zote za maharagwe na jamii ya kunde huwa na protini. Kula hivi badala ya nyama nyekundu na ondoa mafuta yanayoonekana kwenye nyama.

Saba, Unashauriwa usikoboe nafaka. Mfano unga wa mahindi yasiyokobolewa ni bora zaidi kuliko iliyokobolewa. Mikate iliyotengenezwa kwa ngano isiyokobolewa pia nobora.

Nane, unashauriwa kutumia vyakula vyenye vitamini muhimu pamoja na protini kama vile maziwa, mayai na karanga.

Tisa, Kula matunda na mbogamboga kwenye kila mlo kwa ajili ya vitamini, madini na ufumwele.

Kumi, Kiafya mtu anapaswa asitumie zaidi ya kijiko kimoja cha chai kwa siku. Weka chumvi kidogo kwenye vyakula wakati wa kupika. Epuka kuongeza chumvi kwenye mlo wakati wa kula.

Kumi na Moja, Epuka vyakula vilivyo tayari kuliwa kama vya kwenye makopo au vilivyofungwa mitaani. Mara nyingi vyakula hivi huwa na kiwango kilichopitiliza cha chumvi, sukari na mafuta.

Kumi na Mbili, Katika mgawanyo wa vyakula kwenye sahani uwiano unapaswa kuwa; robo ni nafaka au ndizi, robo nyingine ni kunde au nyama na nusu yake iwe ni matunda pamoja na mbogamboga.


Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF). Maoni, ushauri au maswali tuma tjncdf@gmail.com au S.L.P 13695, Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Friday, January 19, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo