Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2018

Mwandishi Wetu
WATU wengi wamekuwa wakipata matatizo ya meno na hata kulazimika kung'oa bila kujua tatizo hilo linatokana na nini na ni namna gani ya kulikabili.

Wengine hujikuta wakitangatanga huko na kule na hata kwenda kwa waganga wa kienyeji lakini matokeo yake tatizo huzidi kuwaandamba.

Ili kujua hatua ambazo unapaswa kuzichukua Dkt. Onesmo Kapugi anaanza kwa kueleza nini maana ya kutoboka kwa meno.

Kutoboka kwa meno ni ile hali ya jino au meno kutengeneza tundu ikiwa ni matokeo ya asidi (tindikali) izalishwayo na bakteria baada ya mtu kula vyakula vyenye sukari.

Meno kutoboka husababishwa na tindikali izalishwayo na bakteria walioko kwenye utando mlaini ambayo taratibu huweza kutoboa jino husika kwa kuanzia kwenye tabaka la nje kabisa la jino na kuzidi kuingia ndani. Kutoboka kwa jino huharibu jino husika ambalo lisipozibwa mapema huweza kuishia kung’olewa.

Meno hutoboka wakati sukari iliyopo kwenye chakula inapotumiwa na bakteria walioko kwenye kinywa ambao kisha hutengeneza tindikali (asidi). 

Kila mara ulapo ama unywapo vitu vilivyo na sukari, tindikali hii hushambulia meno na taratibu huweza kuyatoboa. 

Mashambulizi haya huweza kuchukua hata saa moja baada ya kuwa umekula vitu vya sukari. Ikumbukwe kuwa si sukari tu ambayo ni tishio kwa meno yako, hata vyakula vya wanga navyo ni hatari kwani vinaposagwa huweza kutoa sukari ambayo nayo huchangia kuozesha meno. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.

Hivvo basi kutumia vyakula na vinywaji vya sukari kati ya mlo mmoja na mwingine huongeza uwezekano wa kutoboka meno kwani meno husika huwa yanashambaliwa muda wote na yanakosa muda wa kupumzika. Hivyo ni muhimu kujiepusha na matumizi ya vyakula na vinywaji vya sukari kwa siku nzima.

Dalili za jino kutoboka ni zipi? Kwa kawaida kwenye hatua za awali za utobokaji wa meno huwa hakuna dalili yeyote, isipokuwa jino husika huweza kuwa na alama nyeupe kama ya chaki kwenye eneo ambalo linaanza kutoboka. Alama hii huonwa na daktari wa meno anapokuchunguza ama anapopiga mionzi jino husika.

Mara tu tundu lililoko kwenye jino linafika kwenye sehemu ya kati ya jino (dentine), huanza kuwa na maumivu hasa unapotumia vitu vya baridi, moto vyenye sukari au vya asidi (tindikali).

Maumivu ya jino ni dalili kwamba unatakiwa ukamuone daktari wa kinywa na meno haraka, kwani hiyo huwa ni taarifa kwamba kuna tatizo. Kama usipozingatia madhara yatakua makubwa na inawezekana ukapoteza jino husika ambalo lingeweza kuokolewa kama ungewahi.

Maeneo ya kutafunia chakula na maeneo kati ya jino na jino ndio rahisi zaidi kutoboka. Hii ni kwa sababu mabaka ya vyakula na utando mlaini (Plaque) huweza kujishika katika maeneo haya. Lakini kwa ujumla maeneo yote ya meno huweza kutoboka.

Matibabu ya jino lililotoboka hutegemea hali yake wakati daktari anapoliona kwa mara ya kwanza na kulichunguza kitaalam na kisha kushauriana na wewe.

Je ni mara zote unahitaji kuziba meno? Hapana. Katika hatua za mwanzoni kabisa kama umewahi kwa daktari huweza kuweka kwenye jino linaloanza kutoboka dawa maalumu (fluoride varnish), ili kuweza kusaidia kurudishia madini yaliyopotea kwenye meno. Hata hivyo ni muhimu kufuata mapendekezo ya daktari wa kinywa na meno kuhusu namna ya kujizuia kulingana na hali yako, ili yasianze kutoboka tena.

Kuzuia kutoboka kwa meno
Njia bora kabisa ya kuzuia kutoboka kwa meno ni kwa kupiga mswaki vizuri meno yote usiku kabla ya kulala na pia asubuhi baada ya kula kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya floridi. Hakikisha kwamba unayafikia maeneo yote ya meno wakati wa kupiga mswaki. Fanya flosi ili kusafisha sehemu finyu za kati ya meno ili kusafisha sehemu hizo. Hizi ni sehemu ambazo mswaki wa kawaida haufiki.


Mtembelee daktari wa kinywa na meno mara kwa mara, kadiri atakavyopendekeza. Kwa wastani mtu anatakiwa amuone daktari wa kinywa na meno mara mbili kwa mwaka.

Makala haya yameandaliwa na Jukwaa la Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF). Maoni na ushauri tuma S.L.P. 13695, Dar es Salaam au 0713247889.



Posted by MROKI On Thursday, January 18, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo