Nafasi Ya Matangazo

January 19, 2018

Mwandishi Wetu, TJNCDF

Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Tanzania (TANCDA) linaeleza kuwa moyo na mishipa ya damu ni mfumo wa kusambaza na virutubisho mwilini.

Madhara hutokea iwapo nguvu inayosukuma damu itakuwa juu zaidi ya kawaida na kusababisha shinikizo la damu. Madhara mengine ni kuziba kwa mishipa ya damu.

TANCDA inaeleza kwamba msukumo ukiwa juu sana unaweza kusababisha moyo kushindwa kupiga, kupasuka kwa mishipa ya damu na kusababisha kiharusi au kifo cha ghafla.

Madhara mengine yanayoweza kutokea, yanaelezewa na TANCDA kuwa ni figo kushindwa kufanya kazi.

Mazingira yanayoweza kusababisha mishipa ya damu kuziba inaelezwa kuwa ni mafuta kuzidi katika mfumo wa damu.

Mafuta yanayoweza kusababisha mazingira hayo, TANCDA inayataja kuwa ni yale yanayotokana na wanyama kwani ni rahisi kuganda kusababisha athari kwenye mishipa. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA 

TANCDA inashauri jamii kutumia mafuta ya mimea kwa kuwa ni hayagandi yakiingia kwenye mfumo wa damu kama ilivyo yale yatokanayo na wanyama.

Mishipa mikubwa ya damu ikiziba inaelezewa kuwa inaweza kusababisha kiharusi, shambulio la moyo au miguu kukosa damu na hata kupata gangrini.

Dalili ya shinikizo la damu ni pamoja na maumivu ya kichwa, kizunguzungu, mpapatiko wa moyo lakini mara nyingi inaelezwa kuwa hakuna dalili.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa na kuchambuliwa na TANCDA zinaonesha kuwa kati ya Watanzania 100 wenye umri wa miaka 25 au zaidi, 27 wana shinikizo la damu lakini ni watatu kati yao wanajua wana tatizo hilo.

Tafiti hizo pia zinaonesha kwamba kwa kila watu 100, robo yake, yaani 25 wana mafuta yaliyozidi kwenye mfumo wa damu na wengi wao hawajui.

TANCDA inaeleza kuwa sababu kuu za shinikizo la damu ni pamoja na kutumia kwa wingi chumvi, pombe na kutoshughulisha mwili kwa mazoezi au kazi zinazotoa jasho.

Sababu nyingine zinatajwa kuwa ni matumizi ya njia zote za tumbaku kama vile sigara, shisha, kubwia ugoro na msongo wa mawazo.

Sababu zote hizo zinaelezewa na TANCDA kuwa husababisha mishipa ya damu kuziba na hasa vikiambatana na kuzidi kwa mafuta kwenye mfumo wa damu. 

Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaopambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF). Maoni, ushauri au maswali tuma tjncdf@gmail.com au S.L.P 13695, Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Friday, January 19, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo