Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2018

Mwandishi wetu
TAFITI mbalimbali za hapa nchini zinaonyesha kuwa watu wengi wanaougua saratani huwa hawajifahamu hadi hali zao zinapokuwa mbaya.

Taarifa ya Taasisi ya Taifa ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) inaeleza wagonjwa wengi hufikishwa katika hospitali hiyo wakiwa katika hali mbaya na wengine huwa ni vigumu kupona.

Wanaeleza ya kuwa ni ukweli kwamba saratani nyingi zinaweza kutibiwa kirahisi iwapo mgonjwa atawahi kupata matibabu.

Hii ndiyo kusema elimu ya ugonjwa huo ni ya msingi sana katika kuwafanya watu wawahi hospitali mapema wanapoona dalili za saratani.

Kulingana na wataalamu wa afya, saratani ni ugonjwa unaosababishwa na seli za eneo fulani la mwili kubadili tabia na kuzaliana kwa kasi bila mpangilio na kuathiri utendaji wa mwili.

Zipo saratani za aina nyingi na kila moja ina dalili zake. Mfano ni saratani ya koo, ubongo, damu, kibofu cha mkojo, shingo ya kizazi, matiti na ngozi.

Takwimu za ORCI zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wapya wa saratani wanaofika kutibiwa inaongezeka kila mwaka.

Taarifa za serikali zinaeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea zinazoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani za njia ya mfumo wa chakula na ini, ikilinganishwa na nchi nyingine. BOFYA HAPA KUSOMA MAKALA HAYA ZAIDI

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wastani wa watu 30-35 kwa kila 100,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na saratani ya mfumo wa chakula, koo na ini.

Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2010, ilibainika kuwa miongoni mwa sababu za ongezeko la saratani hapa nchini ni pamoja na mtindo wa maisha usiofaa. 

Utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na mdomo zinasababishwa na mtindo wa kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo. 

Utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Environmental Care ya jijini Dar-es-Salaam mwaka 2013, ulibaini kuwa tatizo la matumizi ya vipodozi visivyofaa pia huchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa ikiwa ni pamoja na saratani ya ngozi.

“Hadi sasa asilimia 52 ya Watanzania wanatumia mkorogo, matokeo yake wengi wameathirika na wanashindwa kuacha. Wengi wa watu wanaotumia kwa wingi vipodozi vyenye sumu ni wanawake,” anasema Euphrasia Shayo, Meneja mradi wa kupambana na vipodozi vyenye sumu katika Shirika la Envirocare.

Saratani si kwamba huwapata watu wazima pekee, bali hata watoto, na katika nchi nyingi saratani ni chanzo kikubwa cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri kati ya miaka mitano na 14.

Takribani asilimia 50 ya watu wanaopata saratani katika nchi zinazoendelea ni wale wenye umri chini ya miaka 65.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani inaeleza kuwa asilimia 30 ya vifo vyote vitokanavyo na saratani husababishwa na mambo matano.

Mambo hayo yanatajwa kuwa ni unene wa kupindukia, ulaji usiofaa hasa kutokupata matunda na mboga kwa wingi, kutokufanya mazoezi, utumiaji wa tumbaku na unywaji wa pombe. 

Mambo mengine yanayochangia ongezeko la saratani hasa katika nchi zinazoendelea ni pamoja na matumizi ya vifaa vinavyotoa mionzi mikali na sumu ya ‘aflatoxin’ inayopatikana katika nafaka zilizovunda wakati wa kuhifadhiwa.

Mambo mengine yanayosababisha saratani ni uchafuzi wa mazingira ya hewa kwa moshi wa tumbaku na wa mabaki ya plastiki.

Vile vile vitu vingine vinavyochochea saratani ni maambukizi ya magonjwa kama vile Virusi Vya Ukimwi (VVU), virusi vya homa ya ini, virusi vinavyosababisha asilimia 90 au zaidi ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) na virusi vya Epstein Barr vinavyosababisha saratani ya uvumbe wa taya kwa watoto. 

Utafiti wa Dk Catherine de Martel na wenzake uliochapishwa mwaka 2012 katika jarida la The Lancet Oncology, unaonyesha kuwa katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 32.7 ya saratani zote hutokana na maambukizi ya vimelea vya magonjwa. 

Vimelea vingine ni Helicobacter pylori wanaosababisha vidonda vya tumbo na wadudu wa kichocho wanaosababisha saratani ya kibofu cha mkojo. 

Kwa wanaume saratani zinazoongoza ni ya mapafu, saratani ya ngozi (Kaposi’s sarcoma), saratani ya tezi dume na saratani ya tumbo la chakula. 

Kwa upande wa wanawake saratani zinazoongoza ni za mlango wa kizazi, ikifuatiwa na ya matiti na ya utumbo. 

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Tanzania, Nsachris Mwamaja anaelezea juu ya gharama za matibabu ya saratani:

“Pale Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), wagonjwa wanaotibiwa bure ni wengi na tiba yao inagharimu fedha nyingi. Kwa mfano mgonjwa mmoja wa saratani huweza kutibiwa kwa Sh. milioni 2. Ndiyo maana kuna changamoto kubwa katika swala hili.”

Wachunguzi wengine wa masuala ya tiba wanasema kuwa, kuna dawa nyingine za saratani ya damu inayowapata watoto zinazogharimu Sh milioni moja mfano dawa aina ya Asparaginase.


Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam.
Posted by MROKI On Thursday, January 18, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo