Nafasi Ya Matangazo

April 27, 2017



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) wakifurahia kuona medali ya dhahabu aliyoivaa Mwanaridha Alphonce Simbu  ambayo aliinyakuwa katika  mashindano ya Mumbai  Marathon nchini India na tuzo aliyoipata hivi karibuni baada ya kushika nafasi ya tano katika mashindano ya London Marathon. Waziri Mkuu alikutana na mwanariaha huyo kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma Aprili 27, 2017.
 *************
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo Aprili 27,2017 limezizima kwa nderemo na shangwe pale alipotambulishwa rasmi mwanariadha Alphonce Simbu, Mshindi wa medali ya dhahabu wa Mumbai Marathon, na moja ya washindi wa London Marathon.

Mwanariadha huyo ambaye pia ni balozi maalum wa DStv, alilitembelea Bunge kama mgeni maalum wa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Harison Mwakyembe akiambatana na muwakilishi wa DStv Johnson Mshana na maafisa kadhaa waandamizi wa Jeshi la kujenga Taifa akiwemo Kanali K.J Mziray – Mkuu wa Utawala na Mafunzo wa JKT

Mara baada ya naibu spika wa Bunge Dk. Tulia Akson kumtaja Simbu, bunge lilizizima kwa shangwe kwa muda  hali iliyoashiria kuraha kubwa kwa wabunge kuweza kumshuhudia mwanariadha huyo ambaye ni tegemeo kubwa la Tanzania katika mashindano ya riadha ya Dunia yatakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu jijini London.

Baada ya ziara hiyo, Simbu alipata fursa ya kusalimiana na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na kisha kuwa na mazungumzo mafupi na Waziri Mwakyembe.

Akiongea wakati wa kupiga picha ya pamoja na Simbu, Waziri mkuu Kassim Majaliwa alimpongeza sana mwanariadha huyo na kusema kuwa  Serikali inatambua na kuthamini sana jitihada zilizofanywa na wadau wote katika kufanikisha ushindi wa Simbu. Pia alimtakia kila la heri katika maandalizi na kisha ushiriki wake katika mashindano ya Dunia yanayomkabili mwishoni mwa mwaka huu.

 Naye Waziri mwenye dhamana ya Michezo Harison Mwakyembe ambaye ndiye aliyemualika Simbu Bungeni, alisema kuwa wizara imekuwa ikishirikiana na wadau kwa karibu ambapo hata wakati wa Safari ya Simbu kwenda London, wizara ilihakikisha safari hiyo inafanikiwa. Ameonyesha kufurahishwa kwake na vipaji vilivyopo na kusema nguvu za ziada zitawekwa ili kuhakikisha kuwa vipaji hivyo vinaibuliwa na kukuzwa kwa manufaa ya taifa zima.

Kwa upande wake, Simbu alisema kitendo cha yeye kualikwa bungeni kimempa faraja kubwa na pia alifurahi sana kuona jinsi wabunge walivyomshangilia na kumpongeza. “Kwakweli ujio wangu bungeni umenipa faraja kubwa kuona ni jinsi gani wabunge wote walivyofurahishwa na mafanikio niliyopata na sifa niliyoiletea nchi. Hii imenipa sana moyo na uzalendo kwani ni dhahiri kuwa taifa zima liko nyuma yangu na linanunga mkono kikamilifu” alisema Simbu

Alitoa shukrani za pekee kwa wadhamini wake DStv, pamoja na Waziri Mwakyembe kwa jitihada kubwa anazofanya. Amesema anaamini kwa mwenendo huu yeye, wanariadha wengine na wanamichezo wote wa Tanzania watafika mbali na hatimaye Tanzania itakuwa kinara katika ulingo wa michezo duniani. Pia alilishukuru Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa kumruhusu kufanya mazoezi na kushiriki katika mashindano mbalimbali.

Simbu ambaye ni miongoni mwa wanariadha bora wa Tanzania alivunja rekodi yake aliyoiweka mwaka jana nchini Japan ya muda wa 2:09:19 na hatimaye katika mashindano ya London Marathon mwaka huu alitumia muda wa 2:09:10 ambao ndio muda wake bora zaidi.

 Simbu ni miongoni wa wachezaji wa timu ya taifa ya riadha watakaoshiriki mbio za Dunia mwezi Agosti mwaka huu jijini London.
Posted by MROKI On Thursday, April 27, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo