Nafasi Ya Matangazo

March 01, 2017

IDADI kubwa ya wahojiwa wa Sauti za Wananchi (asilimia 78) wameripoti uhaba wa chakula katika maeneo wanayoishi. Hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini ambako asilimia 84 wameripoti uhaba wa chakula ikilinganishwa na asilimia 64 katika maeneo ya mijini.

Zaidi ya nusu ya kaya za Tanzania (yaani asilimia 69) zinahofia kuishiwa chakula. Aidha asilimia 51 ya kaya zimeripoti kwamba hakukua na chakula cha kutosha kulisha kaya nzima,  au mwanakaya ameshinda na njaa kwa sababu hakuweza kupata chakula (asilimia 50).

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhtasari  uitwao Uchungu wa njaa: Upungufu wa chakula Tanzania. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia njia ya simu. 

Takwimu za muhtasari huu zimekusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,800 wa Tanzania bara (Zanzibar haikuhusishwa kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 14 na 26 mwezi wa tisa, 2016 na kutoka kwa wahojiwa 1,610 kati ya tarehe 9 na 15 mwezi wa pili 2017.

Kwa mujibu wa wananchi wengi, uhakika wa kupata chakula umepungua kati ya mwezi Septemba 2016 na Februai 2017: Mwezi wa pili 2017, asilimia 65 ya wananchi walikuwa na hofu ya kaya zao kukosa chakula cha kutosha ikilinganishwa na asilimia 45 waliosema hivyo mwezi Septemba 2016. Mwezi Februari 2017, asilimia 51 ya wananchi waliripoti kwamba kuna wakati hawakua na chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Kabla ya hapo, mnamo mwezi Septemba 2016, asilimia 43 ya wananchi iliripoti kwamba hali kama hiyo iliwatokea katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita. 

Mwezi Februari 2017, asilimia 35 ya wananchi waliripoti kuwa na mwanakaya angalau mmoja alieshinda na njaa siku nzima kwa sababu ya kukosa chakula katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Hili ni ongezeko kutoka asilimia 21 walioripoti kwamba hali hiyo iliwatokea katika kipindi cha miezi sita tangu Aprili mpaka Septemba 2016.

Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania zinaonesha kwamba bei ya mahindi (halisi, jumla) imeongezeka mara mbili (baada ya kuirekebisha na kiwango cha mfumuko wa bei wa wakati huo) katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutoka shilingi 400 kwa kilo mwanzoni mwa 2015 mpaka shilingi 852 mwezi wa kumi na mbili, 2016. Wahojiwa wa Sauti za Wananchi wameripoti kwamba kwa wastani kilo moja ya mahindi inawagharimu shilingi 1,253. (Bei zilizoripotiwa kwenye masoko ya ndani).

Upungufu na uhaba wa chakula unaoendelea ni kielelezo cha hali ngumu ya maisha iliyopo na umasikini wa kipato. Jumla ya watu nane kati ya kumi (asilimia 80) wameripoti kwamba kaya zao hazina kipato cha kutosha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
 
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza anasema: “Wananchi wamekumbwa vikali na upungufu wa chakula. Tumepokea mwitikio wa serikali katika suala hili na tunaunga mkono jitihada za kuzuia maafa makubwa. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kwamba wananchi bado wanaishi kwenye hali ngumu na wamejaa hofu ya kukosa chakula. Jitihada za kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania yeyote anayelala njaa zishike nafasi ya kwanza  katika vipaumbele vyetu vya kitaifa.”
Posted by MROKI On Wednesday, March 01, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo