Nafasi Ya Matangazo

March 21, 2017

Maafisa Habari na Tehama kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Katavi na Kagera wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza tovuti za Halmashauri na Mikoa kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) mjini Kigoma.
 Maafisa Habari na Tehama kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Katavi na Kagera wakiendelea na mafunzo ya kutengeneza tovuti za Halmashauri na Mikoa kupitia mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) mjini Kigoma.
Na Nashon Kennedy, Kigoma
MAAFISA habari na Tehama nchini wametakiwa kufanya kazi zao kwa weledi ili kuhakikisha taifa linakuwa na serikali yenye utendaji inayowajibika vyema kwa wananchi wake.
 
Rai hiyo imetolewa mjini hapa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Chalres Pallanjo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku saba kwa Maafisa Habari na watalaam wa tehama wa mkoa na halmashauri kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora  na Katavi yanayofadhiliwa na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma unaojulikana kama Public Sector System Strengthening (PS3).
 
“Kupitia kazi zenu, mnayo dhamana ya kuhakikisha kuwa tunakuwa na Serikali yenye utendaji unaowajibika kwa wananchi wake”, alisema.
 
Alisema hali hiyo itawezekana endapo taarifa sahihi zitawekwa mara kwa mara katika tovuti za halmashauri na zile za mikoa na sio kusubiri hadi wananchi wapige kelele kwa ajili ya kuhoji masuala wanayopaswa kufahamishwa tangu mwanzo.
 
Alisema kwa kipindi kilichopita, maafisa habari na tehama wamekuwa na changamoto ya namna gani ya kuhakikisha kuwa taarifa za maeneo yao zinatoka kwa wakati  lakini pia na utayarishaji wa tovuti kama sehemu ya njia ya mawasiliano.
 
“Ni halmashauri chache zenye tovuti hapa nchini, na hata zile zenye tovuti, bado ipo changamoto ya tovuti hizo kutofanana, kwa maana ya government Website Framework na hivyo kukosa taarifa zingine muhimu”, alisema.
 
Aliushukuru Mradi wa Ps3 kwa kufadhili mafunzo hayo kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) ambapo alisema Tanzania inaweza kuiga mfano wan chi zilizoendelea kama Marekani ambayo imepiga hatua kubwa kwenye mambo ya uwazi na utawala bora kwa kuwapa wananchi taarifa mbalimbali zinazohusu nchi na maendeleo yao.
 
Akitoa mfano, alisema serikali ya Marekani kupitia Ikulu yake imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali kila wiki kupitia kwa wanahabari pamoja na mitandao ambazo zimekuwa zikifuatiliwa na kutumiwa kwa karibu na wananchi wake na duniani kote.
 
“ Huu ni mfano mzuri ambao hata sisi tunaweza kuuiga.  Tuanze basi kulifanya hilo kwa kutumia hizi tovuti katika maeneo yetu”,
 
Kwa upande wake, Mratibu wa PS3 Mkoa wa Kigoma Simon Mabagala alisema lengo la mafunzo hayo kwa maafisa habari na Tehama ni kuiwezesha serikali kuwasiliana na wananchi wake katika masuala na taarifa muhimu za maendeleo kwenye maeneo yao.
 
Naye Mwezeshaji Kiongozi wa Mafunzo hayo Joctan Bikombo alisema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwaunganisha maafisa hao ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili kwa njia ya mawasiliano kupitia tovuti zao.
 
Alisema mafunzo hayo yanafadhiliwa na  PS3 kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na Wakala ya Serikali Mtandao (eGA).
 
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kupata taarifa mbalimbali zinazohusu maeneo yao husika, kama ilivyo haki yao ya Kikatiba.
 
Mafunzo hayo yaliyoanza leo(jana) ambayo ni ya awamu ya pili yanaenda sambamba katika mikoa yote ya Tanzania Bara ambayo haijapata mafunzo hayo na kilele cha mafunzo hayo ni Machi 27 mwaka huu, ambapo halmashauri zote na mikoa zilizo kwenye mafunzo zitazindua tovuti zao kwa pamoja.
 
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, wamesema mafunzo hayo yatawawezesha kupata ujuzi utakaowawezesha kufanya kazi zao kwa haraka na kwa wakati.
 
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Habari wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Gadi Mwatebela alisema ameyapata mafunzo hayo kwa wakati muafaka na matarajio yake ni kujua namna ya kufungua na kutumia tovuti.
 
“Jamii sasa itakuwa na uwezo wa kupata taarifa nyingi za maendeleo za halmashauri yangu baada ya mafunzo haya”, alisema.
 
Kwa upande wake, Afisa Tehama Msaidizi kutoka Halmashauri ya Uvinza mkoani Kigoma Grace Moshi alisema ana matarajio ya kujifunza namna ya kutengeneza tovuti ili awe na uwezo wa kutengeneza tovuti kwenye halmashauri yake.
 
Naye Afisa Tehama kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Halidi Nyange alisema matarajio yake ni kujua namna ya kutengeneza tovuti kwa kuingiza taarifa mbalimbali za maendeleo na kujua namna ya kuboresha tovuti kwa maslahi mapana ya wananchi.
 
“ Matarajio yangu ni kutaka kujua namna ya kujaza au kuingiza taarifa na matukio mbalimbali ya taasisi au halmashauri kwenye tovuti ili kuwawezesha wananchi kupekua na kupata taarifa hizo”, alifafanua.
Posted by MROKI On Tuesday, March 21, 2017 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo